Habari za Punde

NAIBU WAZIRI ATAKA MKANDARASI KUFUATA VIGEZO VYA UJENZI WA MKONGO WA MAWASILIANO

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akiwa ameshika nyaya ya Mkongo wa Taifa na kumuelezea mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Chaurembo (mwenye kilemba) wakati alipozuru katika Wilaya hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano 
 

Na Mwandishi wetu, NANYUMBU

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametoa maelekezo kwa Mkandarasi wa kampuni ya Raddy Fibre anayejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 72 kutoka Mangaka hadi Mtambaswala kuzingatia vigezo vilivyowekwa vya ujenzi wa muundombinu huo ili usiharibu wala kuharibiwa na miundombinu ya barabara za TARURA, TANROAD pamoja na miundombinu ya maji

Maelekezo hayo ameyatoa alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mkongo huo unaoendelea katika wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara kwa lengo la kuimarisha huduma za mawasiliano mpakani hasa kuunganisha mawasiliano baina ya nchi ya Tanzania na Msumbiji

“Mkandarasi yeyote anayepewa zabuni ya kujenga na kuendeleza miundombinu ya Serikali anatakiwa kufanya kazi kwa kufuata masharti ya mkataba na kutoa taarifa sahihi za mradi anaotekeleza ili Serikali iendelee kuwaamini Makandarasi wazalendo kuwa wanakidhi vigezo vya kutekeleza miradi ya maendeleo na kujenga nchi yetu sisi wenyewe”, alizungumza Mhandisi Kundo

Ameongeza kuwa ameona baadhi ya mapungufu katika ujenzi wa Mkongo huo hasa kwa upande wa kina kinachotakiwa kuchimbwa kwa ajili ya kuweka muundombinu huo na kumuelekeza mkandasari kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi na atakwenda kukagua tena ili kujiridhisha

Naye Mbunge wa Nanyumbu Mhe. Yahya Mhata amesema kuwa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaoendelea kufanyika kuanzia Mangaka mpaka Mtambaswala umetengeneza ajira za muda mfupi kwa vijana wa jimbo lake na kuwasaidia kujiingizia kipato ikiwa ni alama kuwa Serikali inawajali wananchi wake

Kwa upande wa Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Raddy Fibre Mohamed Mlanzi amesema kuwa amepokea maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri na kuahidi kufanya maboresho maeneo yote ambayo yanahitaji maboresho

Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la Makanga hadi Mtambaswala una gharama ya shilingi Bilioni 2.4 ambapo kilomita 68 kati ya kilomita 72 zimeshakamilika na kituo kimoja cha kusambaza huduma ya Mkongo kimeshajengwa kwa asilimia 94.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akipima urefu wa kina cha mfereji uliochimbwa kwa ajili ya kupitisha muundombinu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la Maneme katika Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (mwenye suti ya kijivu) akishuhudia mfereji uliowekwa muundombinu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ukifukuliwa ili kujiridhisha kama urefu wa kina umekidhi vigezo katika eneo la Maneme katika Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (mstari wa mbele kulia) akitoka kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kutolea huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la Mtambaswala Mkoani Mtwara. Wengine ni wajumbe alioambatana nao katika ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.