Habari za Punde

Bei ya mafuta yapanda



 Na Mwashungi  Tahir    Maelezo          8-8-2021.

 

BEI ya mafuta ya Petroli, Disel na mafuta ya taa imeendelea kuongezeka kwa mwezi Agosti  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama za uingizaji wa bidhaa hiyo katika bandari ya Dar es Salam.

  

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Mamlaka ya Udhitibi wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Mbarak Hassan Haji, akitangaza bei hizo zitakazoanza kutumika kesho kwa vyombo vya habari Ofisini kwake Maisara, alisema bei ya mafuta ya Petrol, Disel na mafuta ya imepanda ukilinganisha na mwezi uliopita.

 

Aidha alisema bei ya petrol itauzwa kwa shiligi 2,379 kwa mwezi huu kutoka shilingi 2,327  mwezi uliopita tofauti ya shilingi 52 sawa na asilimia 2.23.

 

Alisema mafuta ya Disel yatauzwa kwa shilingi 2,287 kwa mwezi huu kutoka shilingi 2,222 ya mwezi uliopita tofauti ya shilingi 65 sawa na asilimia 2.93.

 

Kwa mafuta ya taa alisema bei ya rejareja itakuwa shilingi 1,711 kwa mwezi huu kutoka shilingi  1,608 ya mwezi uliopita  tofauti ya shilingi 103 sawa na asilimia 6.41.

 

 Aidha akizungumzia sababu zilizopelekea kupanda kwa bei hizo, alisema ni pamoja na kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia, thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola za kimarekani, gharama za usafiri, bima na Premium hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

 

Hata hivyo, alisema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani kwa mwezi uliopita ili kupata kianzio cha kufanyika mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi huu.

 

Sambamba na hayo, alibainisha kuwa licha ya kuwa mafuta yeongezeko lakini yapo ya kutosha kwa matumizi ya Zanzibar kwa mwezi mmoja.

 

Mbali na hayo alisisitiza kwamba ZURA haiamui kupanda na kushuka kwa bei hiyo bali inaangalia vigezo ambavyo vinafanywa kwa uwazi.

 

Hivyo, aliwaomba wananchi kuhakikisha kuwa bei zilizotangazwa ndio bei halalai na kuwasisitiza kununua mafuta katika sheli zilizokuwepo kihalali ili kuepuka kuuziwa mafuta ya magendo na kudai risiti.

 

Sambamba na hayo aliwasisitiza wananchi kudai risiti wanapokwenda kutia mafuta katika sheli.

 

Akizungumzia msisitizo wa wananchi kudai risiti, alisema jambo hilo linasaidia pale mwananchi anapouziwa mafuta yana maji au yana hitilafu yoyote iweze kuchukua hatua.

 

"Lengo letu ni kuona ZURA inawahi kwenye kituo ili kuweza kuchunguza mafuta hayo na kama mwananchi atakuwa hana risiti basi atakuwa hana kielelezo na tutakuwa hatuna cha kumsaidia". alibainisha

 

Mbali na hayo alibainisha kuwa ZURA kwa kushirikiana na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wana mpango wa kuweka masharti ya kila sheli kuweka mashine za kielektronik ili kuona wanaondokana na utoaji wa risiti za mkono.

 

"Tuna mpango huo wa kuhakikisha kila sheli inaweka mashine hizi lakini kuna kanuni ambazo zina taratibu Ili kuweza kuzibadilisha na kuweka sharti hilo kwenye kanuni ambazo zinatakiwa kupata baraka ya waziri na kupitishwa na Mwanasheria Mkuu kabla ya kuanza kutumika," alisema.

 

Mbaraka, alibainisha kwamba mahitaji ya mafuta kwa mwezi yanapanda na kushuka kwani kwa siku mafuta ya petol lita laki 400,000 mpaka  500,000, Disel  200,000 mpaka 300,000 na mafuta ya taa  20,000.

 

Sambamba na hayo aliwaomba wananchi kuacha kunungunika pembeni na badala yake kutumia mifumo iliyowekwa ya kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.