Makamu wa Rais wa Jmuhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Isdor Mpango akihutubia katika hafla ya kusaini hati za makubaliano ya kuondoa hoja za muungano zilizopatiwa ufumbuzi katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA MUSSA _MAELEZO ZANZIBAR.
Issa Mzee – Maelezo
24/08/2021
Jumla
ya hoja kumi na moja zimeondolewa rasmi
katika orodha ya hoja za Muungano na kutiwa saini na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hafla
ya utiaji saini wa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa
ufumbuzi ilifanyika katika ukumbi wa chuo cha utalii Maruhubi nje kidogo ya Mji
wa Zanzibar baina ya Mawaziri wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kati
ya hoja kumi na moja zilizopatiwa ufumbuzi hoja tisa zimesainiwa hati za
makubaliano na hoja mbili ambazo hazihitaji hati za makubaliano tayari
zimepatiwa ufumbuzi wa kuitendaji.
Hoja
zilizosainiwa hati za makubaliano ni pamoja na uvuvi kwenye ukanda wa bahari
kuu, uingizwaji wa maziwa kutoka Zanzibar, ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika
taasisi za Muungano, mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje.
Pia
Mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada
kutoka nje, Mkataba wa mkopo wa mradi wa ukarabati wa hospitali ya Mnazi
Mmoja, Mkataba wa mkopo wa ujenzi wa barabara ya Chakechake hadi Wete Pemba.
Hoja
nyengine ni Mkataba wa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, Usimamizi
wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu unaofanywa na bodi ya
mapato ya Zanzibar na Mapato
yanayokusanywa na uhamiaji kwa upande wa
Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kukamilika zoezi la utiaji
saini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Isdor Mpango
amesema ufumbuzi uliopatikana katika hoja hizo unalenga katika kuhakikisha
maslahi ya pande zote mbili yanapatikana ili kuimarisha Muungano.
Alisema
tukio hilo ni la kihistoria na muhimu kwa mustakabali wa Muungano na
uthibitisho tosha unaothibitisha kuwa kamati inafanya kazi vizuri kwa
kuhakikisha Muungano unaleta maslahi pande zote mbili.
“Maslahi
ya wananchi wa pande zote Zanzibar na Tanzania bara ni muhimu na yanaendelea kuzingatiwa ni vyema
wananchi waelewe ya kwamba serikali zote
mbili zipo pamoja kwa maslahi ya wananchi wote” alisema Dk. Mpango.
Alifafanua
kuwa kamati imeweza kuzifanyika kazi hoja kumi na moja za muungano ndani ya
miaka miwili kutokana na ushirikiano na msingi mzuri ulioekwa na Rais wa Tanzania
mama Samia Suluhu Hassan alipokuwa makamu wa Rais.
Dk.Mpango
alieleza kuwa faida nyingi zitaweza kupatikana, kutokana utiaji saini wa uvuvi kwenye ukanda wa uchumi
wa bahari kuu ikiwemo kupatikana kwa wawekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu,
na kuongeza ufanisi katika sekta ya uvuvi, na ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika
taasisi za Muungano utasaidia kuongeza hamasa kwa wananchi katika kupunguza
uhaba wa ajira.
Aliendelea
kwa kusema, mgawanyo mzuri wa mapato utakaofanyika baina ya pande mbili za Muungano,
utasaidia katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu,
pamoja na kuimarika kwa huduma za afya kutokana na marekebisho ya mkataba wa
mkopo wa mradi wa ukarabati wa hospitali ya Mnazi Mmoja inayohudumia wananchi mbalimbali
nchini.
Aidha
alisema huduma za jamii zitaimarika kwa
wananchi kutokana marekebisho mazuri ya mkataba wa mkopo wa ujenzi wa barabara ya
Chakechake hadi Wete, pamoja na kuiweka Nchi salama kutokana na hatua nzuri iliyochukuliwa
katika mkataba wa mkopo wa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri kwa maslahi ya
kuzilinda mali za Taifa.
“Nia
na madhumuni ya kufanyika hayo yote ni kuuenzi na kulinda Muungano na
kuendeleza udugu uliopo”, alisema Dk.Mpango
Alisema
kuwa hoja nyingi zilizokamilishwa zinahusiana na Wizara za Fedha, kwa pande
zote mbili za Muungano, na kuwataka Mawaziri wenye dhamana ya Wizara hizo
kuzidi kukaa pamoja na kushirikiana katika hatua mbalimbali za kiutendaji.
Vilevile
alisema hoja zote zilizobaki zinaendelea
kutafutiwa ufumbuzi kwa utaratibu mzuri
kwa manufaaa ya pande zote mbili za muungano.
Alitoa
rai kwa taasisi zote zinazohusika kuwa, hoja zote zitafutiwe ufumbuzi na hoja zinazojitokeza zijadiliwe kwa uwazi na
umakini mkubwa ili kuimarisha Muungano.
Nae
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amesema utiaji saini
wa hati za hoja za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa
ufumbuzi baina ya Serikali mbili ni matokeo chanya ya makubaliano yaliyofanywa
na Serikali hizo.
Alisema
makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa kwa maslahi ya Taifa ili kuepusha
migongano kwa kizazi cha sasa na kizazi cha baadae .
Alieleza
kuwa ufumbuzi uliopatikana utawawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao
vizuri bila ya usumbufu wowote nchini.
Aliongeza
kwa kusema, tukio hili litasaidia katika kuwajenga wananchi imani kwamba Serikali zao zinafuatilia vyema
masuala yote yanayohusu Muungano.
Aidha
alitumia fursa hiyo kuwapongeza Mawaziri na Makatibu wote kwa kazi kubwa
walioifanya kwa maslahi ya Taifa.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, alisema
upembuzi na mapitio ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni miongoni mwa kazi kubwa
iliyofanywa na kamati ya pamoja jambo ambalo ni muhimu kwa maslahi ya
watanzania.
Alisema
kuwa hoja mbalimbali zimeweza kupatiwa ufumbuzi katika vikao vilivyofanywa ili
kuimarisha Muungano hivyo ni vyema wananchi wazithamini jitihada za viongozi
wao.
No comments:
Post a Comment