Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Akagua Shamba la Zabibu la Chinangali II Wilayani Chamwino Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua bwawa la Maji la shamba la zabibu la Chinangali II wilayani Chamwino Dodoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la zabibu la Chinangali II  wilayani Chamwino, Dodoma, Agosti  13, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la zabibu la Chinangali II  wilayani Chamwino, Dodoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la zabibu la Chinangali II  wilayani Chamwino, Dodoma, Agosti  13, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua shamba la zabibu la Chinangali II wilayani Chamwino Dodoma, Agosti 13, 2021. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu Mstaasfu, John Malecela na kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendeleza kilimo cha zao la zabibu na kuhakikisha linaleta tija kwa wakulima.

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 13, 2021) alipotembelea mashamba ya zabibu ya Chinangali na Bihawana akiwa katika muendelezo wa ziara zake za kukagua maendeleo ya zao hilo.

 

Aidha, Waziri Mkuu amewashauri wakulima watenge sehemu ya mashamba yao na kulima zabibu za mezani ambazo nazo zina faida kubwa badala ya kulima za kuzalisha mvinyo tu.

 

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Joseph Mafuru ahakikishe anaandaa utaratibu wa kuwasaidia wakulima wa zabibu wa Bihawana kwa kuwawekea mfumo wa umwagiliaji.

 

Waziri Mkuu amesema zabibu zinazopatikana mkoani Dodoma zina thamani kubwa na ni nzuri kwa utengenezaji wa mvinyo ukilinganisha na zabibu zinazolimwa katika maeneo mengine.

 

Amesema kilimo hicho kinamuwezesha mwananchi kuboresha uchumi wake, hivyo amewashauri wakazi wa mkoa wa Dodoma wakiwemo watumishi wa umma wachangamkie fursa hiyo.

 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wakulima wa zabibu kwamba Serikali imedhamiria kuboresha kilimo cha zao hilo kwa sababu kilimo ni mkombozi kwa Watanzania.

 

Amesema Mheshimiwa Rais Samia ameagiza wakulima wasaidiwe kuanzia hatua za awali za uandaaji wa mashamba, upatikanaji wa mbegu, pembejeo hadi hatua ya utafutaji wa masoko.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wizara hiyo ipo katika mkakati wa kufufua shamba la zabibu la Chinangali na tayari wameanza na ukarabati wa mfumo wa maji.

 

Amesema wamefanikiwa kufufua visima vitatu ambavyo vinapeleka maji katika bwawa la umwagiliaji na kwamba wanatarajia kuweka upya mfumo wa umwagiliaji katika shamba lote.

 

Waziri huyo amesema hatua hiyo inatokana na kuharibika kwa mfumo wa awali wa umwagiliaji uliokuwa umefungwa kwenye shamba hilo. Shamba la Chinangali lina ukubwa wa ekari 600 na kati ya hizo, ekari 300 ndizo zimeendelezwa.

 

Pia, Waziri huyo amesema mbali na kufunga upya mfumo wa umwagiliaji, pia wameweka lengo la kuzalisha miche 500,000 kwa ajili ya kupanda upya shamba hilo.

 

 “Kituo cha TARI Makutupora kimeotesha miche mingi ya zabibu za mezani ambayo itagawiwa kwa wakulima ili waweze kupanda kuzalisha aina hiyo ya zabibu kwa wingi.”

 

Naye, mmoja wa wakulima wa zabibu katika shamba hilo, Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela ameiomba Serikali iunde chombo cha kusimamia ubora wa mvinyo unaozalishwa nchini.

 

Awali, Mwenyekiti wa muda wa wakulima wa shamba hilo, David Mwaka alisema wameweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha changamoto zilizosababisha shamba hilo kufa hazijirudii.

 

Alisema ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu watahakikisha wakulima wote wanaolima katika shamba hilo wanalipia gharama za uendaji wa mashamba kupitia mauzo ya zabibu.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 - DODOMA,                      

IJUMAA, AGOSTI 13, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.