Habari za Punde

Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo yasaini mkataba jengo la ghorofa sitaWizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo yasaini mkataba jengo la ghorofa sita

Na Eleuteri Mangi, WSUM, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesaini mkataba wa ujenzi wa jengo la Wizara hiyo awamu ya pili lenye ghorofa sita na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani litakalojengwa eneo la Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini leo Septemba 22, 2021 jijini Dodoma, Dkt. Abbasi amesema jengo hilo litakuwa na ofisi za kisasa pamoja na mahitaji yote yanayohusika katika sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo.

“Jengo hili litakuwa la kihistoria kwa kuwa Wizara hii haijawahi kumiliki jengo la hadhi hii nzuri, matarajio yetu jengo hili litakuwa kichocheo cha sekta hizo kutoa huduma bora na stahili kwa wadau wa sekta na wanananchi kwa ujumla” amesema Dkt. Abbasi.

Aidha, Dkt. Abbasi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo ambazo ni Bilioni 22.843 zipo na zitatolewa kulingana na taratibu za Serikali ambapo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 sawa na miaka miwili kuanzia sasa.

Katibu Mkuu huyo amewahimiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao ni watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo pamoja Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ni wasanifu na wabunifu wa majengo hayo wakamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuwa wao ni mabingwa wameaminiwa kwa uzoefu wao katika masuala ya ujenzi.

Akisisitiza Serikali inavyodhamiria kusimamia sekta hizo, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amesema hadi sasa Serikali imetenga fedha takriban bilioni 9 kuboresha viwanja na kujenga maeneo ya burudani na kupumzikia wananchi, bilioni 1.5 za Mfuko wa Sanaa na Utamaduni, bilioni 1.35 kugharimia timu za Taifa pamoja na bilioni 1.3 kujenga shule ya michezo kitaifa (Sports Academy) katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya mkoani Mwanza.

Serikali inatekeleza hayo yote ikitambua sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo ni nguvu laini ambazo zinatambulisha taifa duniani kwa kazi zake ikiwemo muziki, utamaduni, filamu na michezo na hivyo kuwapa wananchi burudani na furaha hatua inayosaidia kuepuka magonjwa yasiyo ya lazima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani ameishukuru Wizara na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaamini na kuwapa kazi ya ujenzi wa majengo ya Serikali kwa kuwa waliomba na wamepewa kazi hiyo na kuahidi kuitekeleza kwa ubora na kwa wakati kama ilivyopangwa kulingana na bajeti waliyopewa.

Naye Katibu wa Kuratibu Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshaki Bandawe amesema mpango wa Serikali kuhamia Dodoma umerahisisha wizara kuwa na majengo yao na zipo katika eneo moja hatua inayorahisisha wananchi kupata huduma kwa wakati.

Bw. Bandawe ameongeza kuwa majengo ya Wizara yanayojengwa katika awamu ya pili yapo 24 ambapo hadi sasa Wizara nane ikiwemo ya Sanaa, Utamaduni na Michezo zimekamilisha taratibu za ujenzi huo, hivyo zimetekeleza agizo la Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Septemba 08, 2021 la Wizara zote zikamilishe taratibu za ujenzi wa awamu ya pili ifikapo Septemba 30, 2021. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.