Habari za Punde

Tuitumie Vyema Misikiti Ili Kuisaidia Jamii - Mhe Othman Masoud.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akiondoa kipazia kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Masjid Msufini Mwera Wilaya ya Magharibi "A" Unguja na kujumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam katika Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid hiyo baada ya kufungulia.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema, Misikiti ni Taasisi muhimu katika kuhudumia umma na ujenzi wa ustawi bora wa maisha ya jamii, pindipo ikitumika inavyostahiki.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa ‘Masjid Tawheed’, msikiti mpya uliopo Mwera Misufini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Amesema mbali na kuwa ni vituo vya utekelezaji wa ibada, misikiti inahitaji kutumika vyema katika malezi na kupanda mbegu bora ya imani, kutoka kizazi hadi kizazi, kwa kujenga utamaduni bora wa kuwakuza watoto wadogo kwa tabia mbali mbali zikiwemo za kujifundisha kutoa sadaka na kuhudumia umma.

Mheshimiwa Othman, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, ametoa wito kwa waumini kuitunza na kuiendeleza misikiti kwa hali na mali, baada ya juhudi kubwa ya kuijenga, licha ya mazingira magumu ya ukosefu wa raslimali inayowakabili.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, ametoa wito kwa waumini kuitumia misikiti kama njia ya kuepukana na udhaifu wa imani iliyoambatana na dhulma, viapo vya uongo katika umiliki wa mali, na hasa tabia iliyokithiri ya kudai kurejeshewa ‘wanawake’ baada ya kutimia talaka tatu.

Akihamasisha matumizi mema ya mali, Sheikh Mahmoud amesema kuwa ALLAH Ndiye Mwenye mali ambapo matajiri ni mawakala ambao wanahitaji kuitumia katika njia za kheri zikiwamo ujenzi wa misikiti, madrasa na kusaidia wenye shida ya kutafuta elimu.

Akitoa khutba wakati wa Swala ya Ijumaa katika msikiti huo, Khatiib – Sheikh Abdulrahman Al-habshy amesema kuwa pamoja na fadhila nyingi wanazozipata wenye kujenga na kuimarisha misikiti, bali pia kuna haja ya kuigeuza kuwa vituo vya utatuzi wa migogoro katika jamii.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo ambao ni pamoja na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mufti, Sheikh Othman Mohamed Saleh, Rais wa  Jumuiya ya ‘Tears of Joy’ Bw. Jaffar Hussein  ‘Jeff’, Katibu wa Jumuiya ya ‘Fly Family’ Bw. Mohamed Ali Mussa na Wazee wa Mwera Misufini wakiongozwa na Mzee Bakar Ame Mosi.

Msikiti huo umejengwa kwa mashirikiano ya wafadhili mbali mbali ambao ni pamoja na Jumuiya za ‘Fly Family’ na ‘Tears of Joy’, Wamiliki wa Ardhi, Bw. Omar Keis, Bi Zubeida bint Almas na Almarhoum Sheikh Hilal bin Amour bin Rashid.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.