Na Mwashungi Tahir Maelezo
27-10-2021.
Jamii imetakiwa kuwa na mashirikiano na watu wenye ulemavu
ili kuwawezesha kupata haki zao za
msingi na kuweza kujikimu maisha.
Hayo yameelezwa na Afisa Miradi na Utetezi wa Haki za Binaadamu
Ali Yussuf wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Jukwaa la wadau wa Taifa kwa watu wenye ulemavu huko katika Ukumbi wa hoteli
ya Golden Tulip uliopo Malindi katika
ukusanyaji wa taarifa za jumuiya za watu wenye ulemavu 2020.
Amesema jamii iwapo itakuwa karibu na watu wenye ulemavu na kusaidia changamoto zinazowakabili wataweza kufanya
kazi zao kwa ufanisi zaidi na kupata huduma
zote zinazostahiki.
Amesema watu wenye
ulemavu ni sehemu ya jamii hivyo ni vyema kupatiwa huduma zote za muhimu za kijamii
ikiwemo afya, elimu, uwezeshaji ili
kukabiliana na maisha.
Ameeleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikuwajali watu wenye ulemavu kwa kuwawekea miundo
mbinu ya uhakika katika maeneo
mbalimbali kwa lengo kuwarahisishia na kuwaletea maendeleo.
Aidha ameomba kuwekea huduma
lugha za alama katika sehemu zinazotoa huduma za kijamii ili kupata mahitaji
yao bila ya usumbufu na kuweza kufahamika.
“Tunaishukuru Serikali
kwa kuwasogezea huduma muhimu karibu ila vifaa vizidi kusogezwa hasa katika
mambo ya afya”, alisema Afisa huyo.
Nae Mratibu wa Mradi wa
Maendeleo Jumuishi katika Jamii Saida Amour Abdullah amesema iko haja ya kuboreshwa baadhi ya
huduma kwa lengo la kunufaika na mradi
huo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi CHAVIZA
Asha Ali Haji amesema jamii iwe na mwamko wa kuhamasisha kuhusiana na kuwatia
haki za msingi watu wenye ulemavu na
kuacha tabia ya kuwafungia ndani bila ya
kuwapa huduma.
Mradi huo ni wa miaka
mitano katika kila wilaya za Unguja na Pemba ambao umeanza kwa lengo la kuhakikisha kwamba haki za binaadamu zinapatikana inavyotakiwa
kwa watu wenye ulemavu na umefadhiliwa na Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu Norway.
No comments:
Post a Comment