Habari za Punde

Serikali imeiimarisha Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ili kuongeza ufanisi - Dk Hussein Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Uwekazeji Kiuchumi Tanzania ikiwa ni kuelekea katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.(iliyokuwa Tanganyika) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, kuwashirikisha Wawekezaji kutoka Nje ya Nchi na Tanzania
                                 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya nane imechukua juhudi  za makusudi za kuimarisha Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Dk. Mwinyi amesema hayo wakati alipofungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho ya Bidhaa za Viwanda kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport – Zanzibar.

Alisema utendaji wa ZIPA umeimarika  baada ya kuanzishwa kituo kimoja kinachotoa huduma za Uwekezaji (one stop centre), kikihusika na utoaji wa vibali  vya ukaazi, ujenzi, usajili wa kampuni, masuala ya Kodi pamoja na mazingira.

Alisema hivi sasa  Mwekezaji anaweza kupata kibali cha Uwekezaji ndani ya siku tatu endapo atakamilisha vyema taratibu kabla kwenda kituoni, huku akibainisha  malengo ya Serikali ya Mwekezaji kukamilisha usajili huo ndani ya siku moja.

Alieleza kuwa Serikali inakamilisha zoezi la kuwa na Benki ya Ardhi, ikiwa ni hatua ya kutatua tatizo la upatikanaji wa rasilimali hiyo na  kubainisha mipango ya kuwepo maeneo ya ardhi yaliotengwa kwa shughuli za uwekezaji.

Aidha, alisema Serikali imetangaza fursa za Uwekezaji katika visiwa vidogo vidogo kumi vilivyopo Zanzibar, huku zoezi la kuwapata wawekezaji likiendelea.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo  kuendelea kuwahamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza miradi yao  katika sekta mbali mbali, ikiwemo Afya, Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, nishati na miundombinu huku akibainisha uwepo wa fursa kama hizo katika Uvuvi wa Bahari kuu, Viwanda na ujenzi wa nyumba za makaazi pamoja na Biashara.

Akigusia azma ya Serikali kufanikisha utekelezaji wa Uchumi wa Buluu, Dk. Mwinyi alisema Serikali inakaribisha Wawekezaji katika utekelezaji wa miradi mbali mbali, ikiwemo Ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa ya Mangapwani inayojumuisha Bandari ya Makontena, Bandari ya mafuta na Gesi, Bandari ya nafaka pamoja na Chelezo kwa ajili ya matengenezo ya Meli.

Aidha, alitilia mkazo uwekezaji katika kuendeleza Uchumi wa Bahari na kutoa wito kwa Wawekezaji kuwekeza miradi yao kwenye sekta ya Utalii ambayo ina fursa nyingi.

“Lengo letu ni kuvutia Wawekezaji wengi zaidi katika ujenzi wa Hoteli za kisasa na vivutio maalum vya Mikutano ya Kimataifa, tayari yapo maeneo  maalum tuliotenga na tunayoendelea kuyatangaza kwa Wawekezaji”, alisema.

Sambamba na  hillo, alitoa wito kwa Wawekezaji kuwekeza kwenye Uvuvi, hususan uvuvi wa Bahari kuu, akibainisha kuwa bado Bahari haijatumika ipasavyo kutokana na uwekezaji mdogo uliofanyika.

Rais Dk. Mwinyi alisema katika safari ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kumekuwepo na chanamaoto na mafanikio makubwa  yaliopatikana katika utekelezaji wa mipango ya kujenga uchumi, ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Alisema kuanzishwa kwa sheria mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kufanyika kwa maboresho ya baadhi ya sheria kumelenga  kuhamasisha na kulinda Uwekezaji, sambamba na kuvutia Wawekezaji.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandaaji wa Kongamano hilo kwa kazi kubwa na nzuri pamoja na Wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi walioshiriki, ikiwemo makundi kutoka China na Misri.    

Mapema, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekti wa Baraza la Mapinduzi awamu ya sita, Abeid Amani Karume aliwapongeza viongozi wa Serikali zote mbili kwa kuandaa Kongamano hilo lililowajumuisha Wawekezaji na wadau mbali mbali na  kuendeleza juhudi za kuliletea Taifa maendeleo katika nyanja tofauti , ikiwemo kuimarisha uchumi   kwa maslahi ya wananchi wake.

Alisema juhudi za kuvutia Wawekezaji zitaimarisha uchumi pamoja na  kutoa ajira kwa vijana, hivyo akapongeza hatua ya Serikali kuja na Kongamano hilo na kuwashirikisha wananchi wenyewe.

Nae, Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga alisema kumekuwepo hatua kubwa zilizochukuliwa katika kuweka mazingira  bora ya uwekezaji, ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa kitovu cha uwekezaji, kuambatana na Sera na Sheria ziliopo.

Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia masuala ya Uwekezaji  Geoffrey Mwambe alisema Serikali inahitaji shughuli nyingi za Uwekezaji ili kuweza kutoa fursa pana za upatikanaji wa ajira kwa vijana wa Tanzania sambamba na kuwa na walipa kodi wengi.

Alisema kuwepo kwa rasilimali nyingi hapa nchini kunaifanya Tanzania kutokuwa na sababu ya kuwa nyuma kiuchumi, akibainisha faraja iliopo kutokana na Mabenki mbali mbali yaliopo nchini kutumia kikamilifu fursa  ziliopo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa  Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum  Mohamed alisema Kongamanop hilo linatoa fursa kwa Wawekezaji na wadau kutambua fursa za uwekezaji ziliopo katikan Serikali zote  mbili za Muungano.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru  Wawekezaji na wageni wote walioshirki katika Kongamano hilo muhimu kwa mustakbali mwema wa Taifa.

Katika hatua nyengine, Mkurugenzi Mtendaji  kutoka Sekta binafsi Tanzania (Tanzania Private Setor Foundation – TPSF) Francis Nanai, akigusia mchangao wa sekta binafsi, alisema hivi karibuni Tanzania imeridhia mkataba wa Soko Huru Afrika, na hivyo akabainisha kazi  inayoendelea kufanywa na TPSF ya kuwaelimisha Watanzania juu ya jambo hilo, kwa msingi kuwa  itawanufaisha wananchi wote.

Alitoa wito na kuwataka kuwa tayari kwa ushindani, sambamba na kufanya ubia na Wawekezaji mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mkurugenzi  wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar  Hamad Hamad, alisema kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kumeutia nguvu Muungano pamoja na kukuza uchumi na hivyo akabinisha matumaini yake ya kumalizika kwa vikwazo vilivyosalia ambavyo vinasababishwa na watendaji.

Alisema Mamlaka zinazosimamia sekta ya Utalii zina wajibu wa kuwasogeza karibu  wadau wa Utalii, kwa lengo la kukuza utalii wa ndani.     

Katika Kongamano hilo lilowashirikisha Mabalozi, Mawaziri, Wawekezaji na wageni mbali mbali, Dk. Mwinyi alitoa utambulisho kwa Wawekezaji walipaji wakubwa wa kodi pamoja na waliotoa ajira nyingi.

                                                                     

Imetayarishwa na Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.