Habari za Punde

Gati ya Mkokotoni itaufungua Mkoa wa Kaskazini Unguja kiuchumi - Dk Hussein Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ujenzi wa Gati ya Mkokotoni, unalenga kuimarisha utoaji wa huduma ili ziweze kuwa bora na endelevu, sambamba na kuufungua kiuchumi Mkoa Kaskazini Unguja.

Dk. Mwinyi amesema hayo  katika hafla ya  Ufunguzi wa Gati ya Mkokotoni, Mkoa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamra shamra za kutimia miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema ujenzi wa Gati ya Mkokotoni una dhamira ya kuimarisha utoaji wa huduma ili ziweze kuwa bora na endelevu kwa abiria wanaotumia Bandari hiyo pamoja na mizigo mchanganyiko.

Alisema mradi huo unalenga  kuufungua Mkoa huo kiuchumi, wakati ambapo malengo ya Serikali ni kuiboresha zaidi Bandari hiyo ili kuziwezesha meli kubwa kutumia Bandari hiyo, ikizingatia Mji wa Mkokotoni unaendelea kukua kwa kasi kubwa na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

Dk. Mwinyi alisema mradi wa Gati unaolenga kuimarisha shughuli za Bandari utachangia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, sambamba na kurahisisha usafiri wa abiri na mizigo inayoingia na kutoka hapa Zanzibar.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni kutainua Uchumi wa Zanzibar na kurahisha shughuili za wananchi kiuchumi na kijamii.

Aliwaomba wananchi wanaotumia Gati hiyo kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu na akazitaka taasisi zote zitakazofanyakazi katika  Bandari hiyo kufanyakazi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na kujiepusha na vitendo  vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, hususan katika suala la ukusanyaji wa mapato

Aidha, Dk. Mwinyi akawataka Manahodha wa vyombo vya baharini kufuata sheria na mingozo inazotolewa na mamlaka zinazohusika ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Alisema pia Serikali inajikita katika ujenzi wa Bandari ya Mangapwani itakayohusisha Gati mbali mbali ili kuifungua Zanzibar kiuchumi.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa Gati hiyo ni hatua itakayowaletea faraja na kuleta mageuzi makubwa ya kimendeleo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Alieleza kuwa mradi huo umetekelezwa na Serikali kwa asilimia mia moja na kunasibisha hali hiyo kwa kusema  pale patakapokuwepo mipango thabiti, Serikali itaweza kutekeleza miradi mbali mbali (isiyo mikubwa) kwa kutumia fedha zake za ndani bila kutegemea wafadhili.

Aliushukuru Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kuimarisha Bandari ya Mkokotoni na kukamilisha ujenzi wa Gati hiyo ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi, akibainisha kazi nzuri iliyofanyika na inayofaa kuigwa na Wizara nyengine.

Alisema wakati Zanzibar ikiadhimishia miaka 58 ya Mapinduzi, imeshuhudia kuwepo maaendeleeo makubwa ya miundombinu, akibainisha hali hiyo ni kielelezo cha Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuondokana na chanagmoto mbali mbali zinazowakabili.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali iinakusudia kuwaletea maendeleo wananchi wake katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi, huku akibainisha azma ya Serikali ya kuziimarisha Bandari za Malindi, Mkoani na Wete Pemba pamoja na kuanza matayarisho ya ujenzi wa Bandari za Kizimkazi na Shumba Mjini ili kurahisisha shughuli za ukuaji wa kiuchumi na kijamii.

Nae, Kaimu Waziri, Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Leila Kassim Ali alisema kuna umuhimu wa Zanzibar  kuwa na Gati za kisasa ili iweze kupata maendeleo, hususan katika utekelezaji wa  dhana ya Uchumi wa Buluu.

Alisema kukamilika kwa mradi huo  ni kielelezo tosha cha kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, akibainisha Gati hiyo itarahisisha shughuli za ushushaji na upakiaji wa mizigo, sambamba na kuwahakikisha usalama wananhi wanaosafiri kati ya Mkokotoni na Visiwa vya Tumbatu.

Aidha, Waziri wa Nchi 0fisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jaffo alisema kwa kushirikiana  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, atasimamia kikamilifu kuhakikisha changamoto mbali mbali zinazohusiana na masuala yaliomo ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi.

Katika hatua nyengine, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud alisema ufunguzi wa Gati hiyo, utawaondolea kero ya usafiri wnanachi wa Visiwa vya Tumbatu, kuchochea harakati za kiuchumi, kuokoa muda wa safari za baharini kati ya Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania,  na hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuharakisha ufunguzi wa shuguli za Gati hiyo  ili wananchi kupata tija.

Vile vile Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu kupitia tiketi ya CCM, Haji Omar Kheir alieleza kuwa ufunguzi wa Gati ya Mkokotoni ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya 2020 - 2025.   

Alisisitiza umuhimu wa Serikali kusimamia matakwa ya mkataba wa mradi huo kwa kuhakikisha  vyombo vyote vinaweza kufunga nanga  na kufanya shughuli zake  nyakati zote, iwe wakati maji yamekupwa au yamejaa.

Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali  kuhakikisha Boti iliyonunuliwa kwa shughuli za usafirishaji wa wananchi kati ya Mkokotoni na Tumbatu inafanya shughuli zake kikamilifu kwa kuzingatia kuwepo kwa upepo mwingi unaovuma katika kipindi hiki cha Kaskazi, hali inayotishia usalama wa wasafiri.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakar, alitoa taarifa ya kitaalamu kuhusiana na mradi huo na kusema ujenzi wa Gati ya  Mkokotoni  umefanywa na Kampuni ya Ms Edge Engineering Co Ltd chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo (ZBA) na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 6.4.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

 

 

 

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.