Hafla hiyo ya mahafali ya Tisa ya Zanzibar School Of Health iliyofanyika katika uwanja wa Mao Tse Tung Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Hussein Ali Mwinyi kupitia hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Amesema wahitimu hao watasaidia katika jamii na Taifa kwa ujumla katika kuleta Mapinduzi ya Kiafya nchini kwa kusimamia azma na sera ya Afya bora kwa kila mwananchi, ambapo amewataka wadau wa maendeleo kuungana kwa pamoja katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Rais Dr Mwinyi amewaasa wahitimu hao kuendeleza mema yote waliyoyapata chuoni hapo kwa kuzingatia Busara na uadilifu katika kuwatumikia wananchi, na kuwa mabalozi kwa vijana wengine kujiunga na Chuo hicho kwa kupata elimu bora.
Mhe. Dr Mwinyi amewataka wazazi na walezi kuwahimiza vijana kusoma kozi ambazo zina wataalamu wachache nchini, ili kuongeza Idadi ya Wataalamu wenye fani mbali mbali katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Rais Dr Mwinyi ametoa wito kwa Taasisi za Elimu za Juu kuanzisha Programu zinazojikita katika kuunga mkono muelekeo wa nchi kukuza Uchumi wa Buluu, kama ilivyoelezwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025, na kueleza kufurahishwa kwake kwa Jitihada za Chuo hicho Kutaka kuanzisha Shahada ya Ushauri nasihi pamoja na kuanzisha Kozi ya kukabiliana na Majanga.
Aidha ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuwa wa kwanza kuanzisha kozi ya Kukabiliana na majanga akieleza kuwa kozi hiyo ni muhimu kutoka na hali ya kijiografia ya Visiwa vya Unguja na Pemba katika Kukabiliana na Maafa hususan katika Suala zima la Uchumi wa Buluu
Ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa juhudi zao zinazoonekana kwa kusimamia na kukiendeleza Chuo hicho hadi kufikia kuwa na usajili wa kudumu na ithibati kutoka NACTE.
Aidha ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto imejipanga kushirkiana na taasisi mbali mbali katika kunyanyua kiwango cha Elimu nchini na kueleza kuwa Moja ya vipaumbele vya Serikali katika muelekeo wa hali ya uchumi ya mwaka 2021, na kuwataka kutanua mawanda ya elimu nchini ili Chuo hicho kiweze kupanda ngazi na kuwa Chuo Kikuu.
Aidha ameeleza kuwa Serikali ina mradi mkubwa kwa kuongeza miundombinu bora katika sekta ya Afya kwa kujenga Hospital za Mikoa na Wilaya ambapo wakandarasi washaanza kazi hiyo, akieleza kuwa kukamilika kwa majengo hayo kutaweza kutoa fursa ya ajira kwa wahitimu mbali mbali katika fani ya afya
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, wanawake na watoto na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amewataka wahitimu hao kusimamia miiko na maadili ya fani zao katika majukumu ya kila siku ili waweza kutumikia vyema elimu zao.
Mhe. Mazrui amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dr Mwinyi imedhamiria kukuza huduma bora katika Sekta ya Afya ambapo hatua hiyo itasaidia kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi bila ya udhia wowote.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar School Of health Aziza Omar Hamed amesema Chuo hicho kitaendeleza mashirikiano yake na Serikali ili kuhakikisha Azma ya kujenga Zanzibar yenye wataalamu bora katika Fani mbali mbali inafikiwa, na kuzitaka Sekta nyengine binafsi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.
No comments:
Post a Comment