Habari za Punde

Watanzania watumia mwanya wa Uviko 19 kusafirisha madawa ya kulevya

 Na Ahmed Mahmoud

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kelevya (DCEA)imesema kuwa katika kipindi cha Ugonjwa wa Covid-19 baadhi ya watanzania walitumia mwanya huo kujifanya wagonjwa na kwenda kutibiwa nchini India ilhali wakiwa wamebeba dawa za kulevya.

Hata hivyo licha ya kutumia mbinu ya kupata vibali vya kutibiwa nje ya nchi walikamatwa kutokana na intelejensia ya wakaguzi kutoka nchi mbalimbali zinazodhibiti madawa hayo.

Akizungumza jana Jijini Arusha wakati wa utoaji mafunzo kwa watumishi wa idara mbalimbali za serikali jana ikiwa  Uhamasishaji wa  Mradi  wa Upunguzaji Madhara kwa watumiaji wa Dawa za Kulevya Mkoani Arusha, Kamishna Jenerali ,Gerald Kusaya alisema wasafirishaji wa dawa za kulevya wanambinu mbalimbali za kusafirisha dawa hizo lakini mamlaka hiyo imedhibiti.

Alisema katika wimbi la ugonjwa wa covid-19 mwaka jana wasafirishaji walilitumia kusafirisha dawa hizo huku wakijifanya wanaumwa wanakwenda kutibiwa nchini India ilhali wakijua kuwa wanamadawa wanayapeleka huko.

Aliomba watumishi wa afya kuwa makini wanapotoa vibali vya wagonjwa kusafiri kwani inapotokea msafirishaji wa dawa hizo anakamatwa na dawa za kulevya huku amepata kibali cha matibabu kwenda nje ya nchi unashangaa.

"Haiwezekani mtu anaomba kibali kwenda nje ya nchi anapewa halafu katika ugonjwa wa covid-19 anaenda kutibiwa ukimwangalia huyo mgonjwa mwenyewe unajiuliza sana watu wa afya mtusaidie katika hili maana watumiaji wa dawa za kulevya au wasafirishaji wanambinu nyingi na ukiondoka hata Tanzania salama utakamatwa nje ya nchi na dawa zako na kifungo ni maisha au miaka 20 na 30 jela"

Alisema mamlaka hiyo hadi sasa imeshakamata wafanyabiashara wakubwa kadhaa na wengine wanatumikia vifungo magerezani na kusisitiza kuwa Mamlaka hiyo ipo macho usiku na mchana kudhibiti dawa hizo kuingizwa
nchini.

Mwaka jana dawa za kulevya kilo 859 zilikamatwa na kusisitiza kuwa mamlaka hiyo imejipanga vema kukamata dawa mbalimbali zinazoingia nchini ikiwemo bangi na mirungi na ndio maana elimu inatolewa vyuoni na mashuleni ili kudhibiti dawa za kulevya vinazoathiri akili.

Wakati huo huo,Mkuu wa Mkoa wa Arusha,John Mongella alitoa rai kwa jamii kuhakikisha wanatokomeza dawa hizo zinazoua nguvu kazi kwa vijana na kusisitiza kuwa Arusha bado kunachangamoto ya kilimo cha bangi maeneo ya milimani lakini vyombo vya ulinzi na usalama zinapambana ili kudhibiti kilimo hicho sanjari kudhibiti maeneo ya mipakani ikiwemo kwenye njia za usafirishaji kupitia mabasi.

Naye mmoja kati ya warahibu wa madawa hayo,Antony Mambepo alishukuru serikali kwakuweka vituo vya marahibu ili kuwasaidia kupata dawa na kuachana na dawa hizo mbalimbali kwani si aathari kubwa kwa jamii ikiwemo familia zao kwani unaweza ukawa mwizi na kusisitiza watumiaji wa dawa hizo wakienda kwenye vituo watapona na kutoa rai kwa jamii kutowatenga watu hao bali washirikishwe katika ujasirimali ili kujikwamua kiuchumi.

Dk,Jesca Temu ambaye anatoa ushauri wa watumiaji wa dawa za kulevya kwa warahibu alisema Mkoa wa Arusha ni mkoa inayoongoza kwa kesi 189 zilizoripotiwa kwa mwaka 2020 kutokana na hali ya jografia iliyopo kutokana na ulimaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi huku athari za dawa za kulevya ikiwa kubwa ikiwemo ukimwi,homa ya ini na  Uviko -19,ikiwemo athari za uchumi wa kijamii.

Alitoa rai kwa jamii kuhakikisha elimu zaidi inatolewa kuhusu athari za madawa hayo ikiwemo viongozi wa dini ili kudhibiti tatizo hilolinaloleta athari kwa jamii ikiwemo vijana wasomi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.