Habari za Punde

Wajasiriamali Watakiwa Kutenga Muda Wao Kwa Ajili ya Kujifunza Namna Bora Kukuza Bidhaa Zao.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Sharifa Omar Khalfan amewataka Wajasiriamali nchini kutenga muda wao kwa ajili ya kujifunza ili kujua namna bora ya kukuza Bidhaa zao.

Mama Sharif Omar Khalfan ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya siku saba ya Wajasiriamali wa Wilaya ya Magharibi "A" hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Abla Beach Hotel Betrasi Zanzibar.

Amesema mafunzo ni kitu muhimu katika kila hatua ya  maisha ya Mwanadamu  ili kuendana na mazingira halisi na hali ya Dunia ilivyo kwa sasa hivyo ni vyema kwa wajasiriamali kutenga muda kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa biashara zao kwa lengo la kujiongezea kipato.

Mama Sharifa amewataka Wajasiriamali hao kutumia elimu waliyoipata katika kutafuta mbinu na kupanga mikakati thabiti ya utengenezaji wa bidhaa zenye ubora unaohitajika ili bidhaa hizo ziweze kukidhi viwango vinavyoendana na soko la Dunia ndani na nje ya nchi.

Sambamba na hayo Mama Sharifa amesema miongoni mwa mikakati ya ya Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi ni kuwaandalia Wajasiriamali mazingira mazuri ya shughuli zao ikiwemo kuwapatia mitaji isiyo na masharti, kuwasaidia kutafuta masoko ya bidhaa wanazozizalisha pamoja na kuwapatia mafunzo yatakayozisaidia kuzalisha bidhaa zao.

Pamoja na mambo mengine Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wajasiriamali hao kuendelea kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaletea maendeleo na kuwataka kuwa wabunifu katika matumizi ya Tehama ili kuendana na wakati katika kutangaza bidhaa zao.

Aidha Mama Sharifa ametumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Magharibi "A" kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyowalenga wajasiriamali wanawake kwa lengo la kuwainua kina mama kwenda sambamba na lengo la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani amabyo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 ya mwezi wa tatu ya kila mwaka.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Magharibi "A" Mhe. Suzan Peter Kunambi amesema Serikali imeahidi Kuweka miundombinu rafiki kwa wajasiriamali na kueleza kuwa kumetengwa Jumla ya Shilingi Bilioni Moja kwa Wilaya ya Magharibi "A" kwa ajili ya kujenga eneo la kufanyia biashara katika eneo la Munduli na kueleza kuwa Wakandarasi wameshaanza kazi katika eneo hilo.

Aidha Mhe. Suzan amesema juhudi hizo zitaleta mabadiliko katika muda mchache hatua ambayo itamaliza kilio cha muda mrefu kwa wajasirimali wa zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Serikali wa kusimamia Maendeleo ya Viwanda vidogo vidogo na vya kati Zanzibar  (SMIDA) Soud Said Ali amesema wameshiriki katika mafunzo hayo kwa lengo la Kuunga Mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaidia Wajasiriamali kuweza kufikia Tanzania ya viwanda vidogo vidogo na vya kati.

Aidha mbali na Mafunzo hayo ya Wilaya ya Magharibi "A" amesema  wamejipanga kutoa mafunzo hayo kwa Wilaya zote za Zanzibar ili kuwasaidia wajasiriamali kuweza kuwa na bidhaa bora zinazouzika katika soko la Dunia.

Akisoma Risala kwa niaba ya Wajasiriamali walioshiriki katika mafunzo hayo Ndugu Habiba Foum Ali amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa juu ya namna bora ya kutengeneza bidhaa bora pamoja na kutafuta masoko na kujua Usalama wa bidhaa ili ziweze kuuzika katika soko la ndani na la nje hatua ambayo itawapelekea kujiajiri pamoja na kuajiri wengine.

Mafunzo hayo ya siku saba yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi "A" kwa kushirikina na Wakala wa Serikali wa kusimamia Maendeleo ya Viwanda vidogo vidogo na vya kati Zanzibar  (SMIDA)  yamejumuisha wajasiriamali Wanawake thamini kutoka Wilaya ya Magharibi "A" ni katika Shamra shamra za kuelekea siku ya Wanawake Duniani.

Awali Mama Sharifa Omar Khalfan alipata fursa ya kukagua na kujionea shughuli mbali mbali za Wajasiriamali waiobahatika kupata mafunzo hayo.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya makamu wa pili wa rais wa Zanzibar

05/03/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.