Habari za Punde

ANNA MGHWIRA CCM ILILAMBA GARASA

 
Na.Adeladius Makwega–DODOMA

Ukiwa kijijini unaweza ukawa na kuku wako wengi majogoo kwa temba (tetea), majongoo yako yanaweza yakawa yanapanda vizuri na tetea zako wanataga, kuyalalia na hata kutotoa vifaranga vizuri mno lakini ukautamani uzao wa jirani yako, ukachukua kuku kwake uende kuwafuga kwako ili kuongeza uzao wa kuku wako.

Kinachokufanya kuchukua kuku wajirani tamaa ya kibinadamu kwa hiyo unapoleta kuku mgeni katika banda lako kuna mambo makubwa mawili unaweza ukawa wa manufaa lakini inawezekana ikawa vinginevyo.

Anachokifanya mfugaji huyu wa kuku kinaweza kulingana na mchezaji wa karata, (Carta-Kireno, Karatasi-Kilatini, Cards-Kiingereza) Hasahasa mchezo wa Arubasitini. Katika mchezo huu mchezo wa sitini na nne, huwa kuna karata 36 unachezwa na watu wawili, wanne au sita ambapo ulaji wa karata hutegemea karata inayotawala mchezo (Alalae) na mshindi hupata alama zaidi ya 60 (Wahedisitini).

Katika mchezo huo unapopata karata inayotawala mchezo (Alalae) au kupata karata dume, jike la karata nyingine ukicheza vizuri zina faida kusaidia kupatikana kwa mshindi. Lakini yule anayeshindwa katika mchezo inawezekana akapuna magarasa ambazo ni karata zisizo na thamani yoyote ile, mtu huyu huambulia patupu.

Mei, 18 2017 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Meck Sadiki alijiuzulu na Rais Magufuli aliliridhia kujiuzulu huko na Juni 3, 2017 akamteuwa Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa huo. Kukiwa na hoja mbona mpinzani kateuliwa? Wengi wakiwa hawafahamu uwezo wa mama huyu.

Kwa maeneo mengi wakati huo suala la elimu bure lilikuwa linasumbua sana, maneno kama msitoe michango, sera ya serikali ni elimu bure yalisemwa.

Maeneo mengi ya Tanzania kelele zilipigwa mno lakini sikusikia Mkoa wa Kilimanjaro, ikanibidi nianze kufuatilia hivi huku Kilimanjaro mbona kelele za elimu ya bure za kukataa kuchangia elimu sizisikii?

Nina rafiki yangu mmoja nilisoma naye zamani yeye akiwa Zanaki mimi nilikuwa Tambaza sasa ni mwalimu sekondari, mkoani humo.

“Mwanzoni jambo hilo lilikuwa gumu sana, lakini viongozi wa dini walishirikishwa vizuri mno, jambo hilo likaeleweka vizuri sana, ikiwa kila Jumapili Kanisani, kila Ijumaa Msikini matangazo ya kusisitiza michango ya elimu yalitolewa- hoja wazazi wote kulipa pesa ya chakula cha mchana shuleni.”

Zikaundwa kamati za wazazi za shule ambazo zilikuwa zinasimamia suala hilo, wanakusanya fedha, wananunua chakula wanawapikia watoto wao na kuwagawia wenyewe.

Wamefungua akaunti zao, wanayasimamia mambo yao wenyewe, wanafunzi wanapikiwa kande na siku zingine wanapikiwa mseto wa mchele na maharagwe badala ya wanaunzi kutoka shuleni saa nane walianza kutoka saa kumi jioni na hata muda wa kusoma uliongezeka.

Walikwenda mbali mno viongozi wa dini wa mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana wakisema waumini/washirika nendeni mkatoe pesa ya chakula cha mchana cha watoto wenu shuleni, usijidanganye kuja kutoa sadaka wakati mtoto wako haujamlipia pesa ya chakula cha mchana shuleni. Kwa hakika Mashekhe, Mapadri na Wachungaji walifanya kazi kubwa mno katika hilo.

“Hata kama elimu bure, hao wanaonadi elimu bure mnadhani wanaweza kumnunulia sare za shule mwanao? Hata kama elimu bure, hao wanaosema hivyo wanaweza kumnunulia mwanao chakula cha mchana? Hata kama elimu bure, hao wanaopaza sauti juu ya hilo wanaweza kumnunulia mwanao madaftari ya kuandikia shuleni?”

Viongozi wa dini waliingia hadi katika kamati za shule hizo mathalani kuna shule inaitwa J.K Nyerere Moshi Mjini miongoni mwa wajumbe wa kamati ya shule ya chakula ni Mchungaji Nkya ambapo anaongoza Kanisa Kiinjili la Kilutheri Ushariki wa Majengo.

Niliumwa sikio kuwa Mama Anna Mghwira alikuwa na PHD ya theolojia kwa hakika alitumia elimu hiyo kujenga ushirikiano na viongozi wa dini na kweli chakula cha mchana mashuleni mkoa huo si tatizo tena na wazazi waliitikia.

Japokuwa Mama Mghwira amefariki lakini Kilimanjaro itaendelea kunufaika na chakula cha mchana mashuleni kwani nina hakika wanafunzi wa mkoa huo wataendelea kufanya vizuri zaidi na zaidi kitaaluma.

Natambua yapo maeneo yalijaribu kuhamasisha hilo lakini mwisho wa siku waliogopa pengine kutumbuliwa, wakakaa kimya, kimya kabisa kama maji ya mtungini na hata shule zilizokuwa zinakula chakula cha mchana zikaacha huo mtindo. Nakuuma sikio msomaji wangu mie shule za kwetu wanakula vizuri wali maharage na muda mwingine wali na kunde.

Maswali ubaoni ni haya, Je wewe kama kiongozi wa kata, shule zako wanafunzi wa kutwa wanakula chakula cha mchana shuleni? Wewe mbunge wa jimbo, je jimboni kwako wanafunzi wa kutwa wa shule za umma umehamasisha wazazi wachangie watoto wao wale chakula cha mchana shuleni? Wewe mkuu wa mkoa katika mkoa wako ni shule ngapi za umma zinakula chakula cha mchana shuleni?

“Hapa ndipo anapozaliwa Katibu Mkuu wa wizara … na shule ile ndiyo kasoma.” Ukienda hapo uliza je wanafunzi wanakula chakula cha mchana shuleni? Jibu lake hawali. Ukifuatiliwa ndugu hao katika fomu zao za likizo wanakwenda makwao, basi ninawauma sikio jamani muende kuhamsisha watoto wetu wale chakula cha mchana shuleni kuongeza virutubisho mwilini na kukuza uelewa ili wafanye vizuri kimasoma tupate makatibu wakuu na maprofesa wengine kutoka eneo hilo.

Mama Mghwira amefariki huku akiacha shule zote za umma za kutwa Kilimanjaro wanakula chakula cha mchana, hilo ni jambo kubwa la ustawi wa maisha ya binadamu na kama mambo yaharibika basi ni sasa, narudia tena kama mambo yaharibike basi ni sasa.

Kumbe uteuzi wa Mama Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ilikuwa ni sawa na kupata karata ya mchezo (alalae) kwa Arubasiti na pia kama mfugaji wa kuku basi tetea wetu alitaga, kuyalalia na kutotoa mayai yote na vifaranga vyote vi hai vinakuwa salama.

Natambua fika siyo ukichukua kuku wote wa jirani watafanya hivyo, kama Arubasitini mwanakwetu unaweza ukalamba magarasa, kumbuka magarasa huwa mengi kuliko madume, jike, mzungu wa nne, mzungu wa tatu na mzungu pili.

Mwanakwetu nahitimisha kwa kusema kuwa kwa Anna Mghwira CCM ya Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro haikulamba garasa.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.