Habari za Punde

Uzinduzi wa Jumuiya ya mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu Zanzibar (JMVUZ)

Mkuu wa Idara ya sheria Chuo cha mafunzo Zanzibar Yussuf Maabad Makungu (aliyesimama) akizungumza na wadau walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Jumuiya ya mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu Zanzibar (JMVUZ) iliyofanyika ukumbi wa Chuo cha mafunzo Kilimani mjini Zanzibar.

NA MALEZO ZANZIBAR 01.04.2022

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeombwa kuanzisha mchakato wa kutoa Vyeti maalum kwa wahitimu waliopitia mafunzo wakiwa wanatumikia kifungo katika vyuo vya Mafunzo nchini ili viwasaidie katika fursa za Ajira.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya sheria Chuo cha mafunzo Zanzibar Yussuf Maabad Makungu katika hafla ya uzinduzi wa Jumuiya ya mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu Zanzibar (JMVUZ) iliyofanyika ukumbi wa Chuo cha mafunzo Kilimani mjini Zanzibar.

Amesema Wanafunzi wa Vyuo vya mafunzo wameandaliwa utaratibu maalum unaowawezesha kujifunza fani za nyanja tofauti, hivyo ni vyema Fani zao kutambulika kwa kupewa Vyeti pale Kesi zao zinapomaliza na kurudi uraiani. 

Maabad amesema ni jambo la kupongezwa kuwa na Jumuiya iliyowakusanya pamoja watu walioingia katika mfumo wa kijinai na kuhukumiwa lakini wakaweza kuanzisha chombo cha kuwasemea na kupigania maslahi yao.

Kwa upande wake Said Suleiman Ali Mratibu wa Jumuiya ya mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu Zanzibar (JMVUZ) amesema malengo ya Jumuiya ni kuhakikisha vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wa makundi mbalimbali vinaondoka Zanzibar.

Amesema mapambano ya kuondoa uhalifu kupitia Jumuiya yao yatajikita zaidi katika kurekebisha tabia za wanajamii kwa kueleza mambo mbalimbali yanayoweza kuwapelekea watu kupata hukumu ya kifungo.

Amefahamisha kuwa wanachama wengi wa Jumuiya hiyo ni wale wote waliowahi kuhukumiwa vifungo au kukaa rumande kwa zaidi ya miezi sita.

“Kwa vile wanachama wetu wengi ni wale waliowahi kupata hukumu ya kifungo, bila shaka watakuwa na ushuhuda mwingi wa kuieleza jamii ili nao waepukane kufanya matendo ya kihalifu” alisema Mratibu Said.

Amesema wafungwa wanapokuwa katika vyuo vya mafunzo hukumbana na mengi ikiwemo kukosa huduma zao muhimu hivyo, Jumuiya itakuwa mstari wa mbele kutetea maslahi na haki zao wanapokuwa ndani au nje ya vyuo vya mafunzo.

Said amesema jambo jingine watakalolipa kipaumbele katika Jumuiya hiyo ni kuhakikisha wanatoa msaada wa kuwapatia Wanasheria na Mawakili ili kuwatetea wanachama wao.

Amesema wanakusudia pia kupambana na dhana mbaya iliyojengeka katika jamii dhidi ya watu waliowahi kupitia vyuo vya mafunzo na kunyooshewa vidole pale wanapopita mitaani.

“Fikiria Mtu anahukumiwa kifungo cha miaka 30, bila shaka kila jambo lake hukaribika. Akirudi mtaani anaanza maisha upya yaliojaa ugeni. Sisi kama Jumuiya lengo letu ni kukutana na watu hao kuwajenga vyema kimawazo ili wakitoka wasiwe wageni wala wasitengwe” Alisema Mratib Said.

Amefafanua kuwa kukiwa na uhalifu katika jamii, usalama wa Zanzibar hutetereka hivyo wanapopambana na uhalifu wataisaidia Serikali kupunguza rasilimali watu, fedha na vifaa ambavyo vingetumika kupambana na uhalifu.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana nao kwa kuwapa mbinu ambazo zitasaidia kutimiza malengo waliojiwekea.

  IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.