Na. Mwandishi Wetu
Kamishna wa Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) Ndg. Yusuph Juma Mwenda amewaasa washauri wa kodi
kutojihusisha na kuwasaidia walipakodi katika kukwepa kulipa kodi stahiki
Serikalini akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya taaluma yao
na sheria za nchi.
Kauli hiyo ameitoa
mara baada ya kukutana na washauri wa kodi katika mkutano wa siku moja uliofanyika
katika ukumbi wa mkutano wa jengo la ZRB Mazizini Zanzibar.
Kamishna huyo amesisitiza
kuwa ili washauri wa kodi wawe weledi katika ufanyaji wao wa kazi ni lazima
wafanye kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa pamoja na
kujipambanua baina ya Serikali na walipakodi ili kuhakikisha kuwa mapato ya
Serikali yanapatikana ikizingatiwa kuwa kiwango cha ulipaji kodi wa hiyari bado
hakiridhishi Zanzibar.
Alisema kuwa, taaluma
ya Ushauri wa Kodi ni taaluma muhimu kwa maendeleo ya nchi na kwamba wanapaswa
kuwa Daraja muhimu baina ya Serikali na Walipakodi ili kufanikisha maendeleo ya
nchi.
Pamoja na kufurahia
mkutano huo ambao ni wa mwanzo kwa Kamishna na washauri hao, Washauri wa kodi waliorodhesha
changamoto kadhaa za kiutendaji ambazo walimshauri Kamishna na uongozi wake
kuzifanyia kazi ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Ikiwa ni katika
kuchapuza uweledi wa washauri hao, ndugu Mwenda ameahidi kuyapatia ufumbuzi
ndani ya kipindi kifupi changamoto za ukusanyaji zilizopo ZRB kwa kufungua
ofisi za Mikoa Pamoja na kuwaongezea ujuzi watendaji wa taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment