Habari za Punde

Mwanazuoni Aliefariki Miaka 100 Iliopita Sheikh.Al-Habib Sayyid Ahmad bin Sumait Kukumbukwa Zanzibar. Kwa Kisomo Msikiti wa Ijumaa Malindi Unguja.

 

ZAIDI ya Wanazuoni 38 wa dini ya Kiislamu kutoka nchi tano wanatarajiwa kuwasili Zanzibar kuanzia wiki ijayo kushiriki kumbukumbu ya karne moja tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa Mwanazuoni maarufu Afrika ya Mashariki na Kati, Sheikh Al-habib Sayyid Ahmad bin Sumait mwaka 1925.

Msimamizi wa mkuu wa shughuli hiyo, Shekhe Mohamed Omar Alsheikh  alisema juzi mjini hapa kuwa, tukio hilo litahudhuria na wanazuoni kutoka katika nchi za Comoro, Kenya, Yemen, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kenya na Uingereza.

Aliwataja baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa kidini watakaohudhuria shughuli hiyo ni, Mufti Mkuu wa Comoro, Sheikh Abubakar Abdallah Jamalullayl na Kadhi Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh  Muhammed bin Othman.

Sheikh Alsheikh aliwaeleza waandishi wa habari kuwa  kumbukumbu ya Mwanazuoni huyo itaanza wiki ijayo Mei 12 hadi 16 kwa kuanza na kisomo cha Maulid (hauli) itakayofanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Malindi ambapo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi atahudhuria.

Alisema ujumbe wa Wanazuoni hao pia utakutana na viongozi wengine wa kitaifa pamoja na kuhudhuria mihadhara mbalimbali ya kidini.

''Kwa muda wa wiki moja tutakuwa na ugeni wa viongozi na wanazuoni wa dini ya Kiislamu ambao watahudhuria kumbukumbu ya karne moja ya kifo cha Mwanazuoni maarufu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi atahudhuria,'' alisema.

Historia ya Mwanazuoni huyo  Sheikh Sumeit inaoneshwa kwamba, alizaliwa Januari 17, mwaka 1861 katika Kisiwa cha Ngazija (Comoro) ambapo nasaba yake inatokana na Mtume Muhammad (SAW) kupitia mjukuu wake Sayyidna Hussein bin Aliy bin Abi Twalib.

Aidha, kumbukumbu zinaonesha kwamba, Sheikh Sumeit aliwahi kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar kipindi cha utawala wa Sultani Barghashi bin Said mwaka 1883 akiwa na umri wa miaka 22, ambapo ilipofika mwaka 1886 aliacha kazi na kwenda nje kwa masomo zaidi.

Mwaka 1888 baada ya kurudi masomoni aliendelea na wadhifa wake wa Kadhi Mkuu wa Zanzibar chini ya utawala wa Sultani Khalifa bin Said hadi ilipofika mwaka 1925. 

Sheikh Alsheikh aliwataka Waislamu kujitokeza kwa wingi kuhudhuria kisomo hicho pamoja na kupata mawaidha yatakayotolewa na viongozi hao wa kidini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.