Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuendeleza Utiifu na Tabia Njema Walizokuwa Nazo Kipindi cha Mwezi wa Ramadhani -Alhaj.Hussein Mwinyi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia Baraza la Eid Fitry katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Unguja Jijini Zanzibar leo 3-5-2022, baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewanasihi wananchi kuendeleza utiifu na tabia njema walizokuwa nazo katika kipindi chote cha mwezi wa Ramadhani kwani ni msingi muhimu wa kudumisha amani, utii wa sheria na utawala bora.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya Baraza la Idd El Fitr lililofanyika huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Alhajd Dk. Mwinyi alisema kuwa ni wajibu kuendelea kuhimizana na kukumbushana umuhimu wa kuyaendeleza mambo mazuri yaliyokuwa yakifanyika na kufundishana katika kipindi chote Ramadhani, kwani Mwezi wa Ramadhani ni msimu maalum wa kujifunza uchaMungu kwa kufanya mambo mema na kujiepusha na makatazo yake.   

Katika hotuba yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kuwa miongoni mwa mafunzo muhimu yaliyopatikana katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni moyo wa mapenzi na kuhurumiana kwa kuwafikiria na kuwafanyia ihsani waliokuwa na mahitaji mbali mbali.

Aliongeza kuwa Taasisi na Waislamu mbali mbali walihamasika na kuwapatia sadaka na misaada mbali mbali wale waliokuwa na uwezo mdogo wa kukidhi mahitaji yao, wakiwemo mayatima, wajane, wazee na watu wenye ulemavu.

“Kwa hivyo, nasaha zangu ni kwamba  hata baada ya kukamilika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wajibu wetu kuendeleza mwenendo huo mwema”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa Uislamu unafundisha kuwa utoaji wa zaka na sadaka kwa wanaostahiki una faida nyingi zikiwemo kuitakasa nafsi ya mtoaji na kuleta mapenzi katika Jamii ambapo pia, utoaji wa zaka na sadaka huondoa chuki, husda na uadui na una mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye mapenzi na udugu wa kweli, na kuhamasisha ushirikiano ndani ya jamii. 

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzipongeza taasisi mbali mbali na Waislamu walioandaa mashindano  ya kuhifadhi na kusoma Qurani.  Hii ni ibada yenye fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini pia ni njia nzuri ya  kuwatayarisha Masheikh na Maulamaa  wa baadae kutoka katika wasomaji hao.

Kwa kuzingatia kuwa sikukuu ni furaha na sikukuu ni amani, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi wenzake na walezi kuzingatia usalama wa watoto wetu hasa katika kipindi hichi cha sikukuu.

Alisisitiza kwamba wote hao wana wajibu wa kuwasimamia na kuhakikisha watoto wapo salama dhidi ya mambo yote yanayoweza kuharibu furaha na amani yao pamoja na sisi wazazi.

Sambamba na hayo, aliwahakikishia wale wote wanaojiandaa kwenda kutekeleza ibada ya Hijjah kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Wakfu na Mali ya  Amana na Wizara ya Afya zitawapa ushirikiano ili waweze kwenda kutimiza nguzo hiyo  muhimu ya Kiislamu kwa kila mwenye uwezo.

Aliongeza kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana na Wizara ya Afya zitawapa ushirikiano ili waweze kwenda kutimiza nguzo hiyo muhimu ya Kiislamu kwa kila mwenye uwezo.

Alilihimiza Jeshi la Polisi kuongeza nguvu katika kusimamia usalama barabarani, hasa katika kipindi hiki cha Sikukuu kwanin ni vyema kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia kupunguza ajali za barabarani na msongamano wa gari, tatizo ambalo linajitokeza sana hivi hasa katika siku za sikukuu.

Waendesha vyombo vya abiria  nao alitakiwa kuwa makini katika kipindi hichi chote cha siku za sikukuu ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Akimkaribisha Alhaj Dk. Mwinyi kuzungumza na wananchi, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Alhaj Haroun Ali Suleiman alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza utamaduni huo huku akitumia fusra hiyo kueleza kwamba Ubalozi wa Saud Arabia mwaka huu umeridhia waumini kote duniani kwenda kufanya Ibada ya Hijjah nchini humo na kutoa nafasi 1400 kwa Tanzania.

Mapema Rais Dk. Mwinyi aliungana na Waislamu mbali mbali katika Sala ya Idd El Fitri Kitaifa iliyosaliwa katika Masjid Zenjbaar, Mazizini Mjini Zanzibar ambapo akisoma hotuba ya Sala hiyo Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume aliyaeleza mafunzo ya Ramadhan huku akiwasisitiza waumini pamoja na wananchi kuendelea kuomba dua ili uchumi wa Zanzibar uzidi kuimarika.

Baada ya hapo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na viongozi wa dini pamoja na baadhi ya Masheikh kutoka sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba kwa ajili ya kuomba dua ambapo Alhaj Dk. Mwinyi aliwapongeza kwa juhudi zao walizozichukua katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kusomesha darsa na miongozo mengine ya dini pamoja na kuiombea nchi idumu kuwa na amani.

Sambamba na hayo, akiwa katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar Alhaj Dk. Mwinyi alitoa mkono wa Idd kwa kuwagaia skukuu wananchi mbali mbali waliofika viwanjani hapo.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.