Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China za kuiunga
mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Rais Dk.
Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar, katika mazungumzo kati yake na Timu
ya Madaktari Bingwa kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China ambao wanatoa huduma
katika hospitali za hapa Zanzibar, mara baada ya kukabidhiwa na Timu hiyo dawa
pamoja na vifaa tiba mbali mbali.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba kwa kipindi kirefu Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
afya kwa kusaidia vifaa, dawa na hata Madaktari ambao wamekuwa wakija Zanzibar
kutoka nchini China kila mwaka.
Rais
Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Timu ya Madaktari 21 kutoka China ambao wanatoa
huduma za afya hapa nchini hivi sasa na kueleza kwamba misaada yao hiyo pamoja
na huduma wanazozitoa zinasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa Madaktari
Bingwa, dawa pamoja na vifaa tiba katika hospitali za hapa Zanzibar.
Aidha,
Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Timu hiyo ya Madaktari kwa kutoa huduma za
afya zikiwemo zile za upasuaji wa kutumia teknolojia ya kisasa ambazo zimeweza kusaidia
kuimarika kwa huduma za afya nchini.
Rais
Dk. Mwinyi alieleza kufarajika na juhudi zinazochukuliwa na Timu hiyo ya
kuwasomesha Madaktari wazalendo ambao wanatoa huduma za afya katika hospitali
kadhaa za Unguja na Pemba.
Sambamba
na hayo, alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar za kuweka mazingira mazuri katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa Hospitali za Wilaya unaoendelea hivi sasa, hali ambayo
itaimarisha zaidi huduma za afya Unguja na Pemba.
Nae
Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui alieleza jinsi mashirikiano makubwa yaliopo
kati ya Wizara yake pamoja na Timu hiyo Madaktari wanaotoa huduma zao katika
hospitali za hapa Zanzibar huku akieleza kwamba dawa pamoja na vifaa tiba hivyo
vina gharama ya zaidi ya TZS Milioni 300.
Mapema
Kiongozi wa Timu hiyo ya Madaktari Bingwa kutoka China Dk. Qu Li Shuai alimueleza
Rais Dk. Mwinyi juhudi zinazochukuliwa na timu hiyo yenye Madaktari 21 ambao
kati ya hao 12 wanatoa huduma katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na 9 wanatoa
huduma katika hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba.
Akitoa
ufafanuzi juu ya misaada hiyo, Bwana Song Jianqing alimueleza Rais Dk. Mwinyi
kwamba msaada huo ni muendelezo wa utamaduni wa uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na China ambao umewekwa na waasisi wa nchi mbili
hizo.
Bwana
Jianqing alieleza kwamba Timu hiyo ya Madaktari ambayo iliwasili Zanzibar mnamo
mwezi Septemba mwaka jana imeanza
kufanya kazi vizuri na tayari imeshatibu zaidi ya wananchi 50,000 na kuwafanyia
upasuaji zaidi ya wagonjwa 6,000 katika hospitali za Mnazi Mmoja, Abdalla Mzee na Kivunge.
Alieleza
kuwa katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo Timu
hiyo ya Madaktari Bingwa wameanzisha mafunzo kwa Madaktari wazalendo hatua
ambayo itazidi kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.
Aidha,
alieleza jinsi walivyofanya upasuaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa hapa
Zanzibar ambayo ni ya kwanza kufanyika katika hospitali za hapa Tanzania.
Aliongeza
kuwa tayari wameshafanya pasuaji kadhaa zikiwemo za koo, masikio, macho,
uchunguzi wa mfumo wa njia ya chakula na nyenginezo ambazo hapo mwanzo huduma
hizo zilikuwa zikipatikana Tanzania Bara.
Alivitaja
miongoni mwa vifaa hivyo kuwa ni ECG defibrillator, potable echocardiography
machines, probes, Trocar kwa ajili ya upasuaji wa laparoscopic, video ya laryngoscope,
electric negative pressure suction devices, oxygen generators, multifunctional
monitors, mesh, surgecal sutures na vyenginevyo.
Imetayarishwa na Idara ya
Mawasiliano,
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment