Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amewataka Wanachama wa CCM Kuwachagua Viongozi Madhubuti Wenye Uwezo Kikivusha Chama Katika Uchaguzi Mkuu Ujao 2025.

 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akipiga Kura kumchagua Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kilimani na Wajumbe wake, uchaguzi huo uliofanyika leo 5-6-2022, katika ukumbi wa Tawi hilo Kilimani Wilaya ya Mjini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Dk. Hussein Ali  Mwinyi amewataka wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuchagua Viongozi madhubuti wenye uwezo wa kukivusha chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika salamu  alizotoa kwa wanachama na Viongozi wa tawi la CCM Kilimani  baada ya kukamilisha zoezi la kupiga kura ; katika uchaguzi wa kuchagua Viongozi mbali mbali wa Tawi hilo  ngazi ya Tawi.

Alisema jukumu kubwa la chama cha Siasa ni kushika Dola, hivyo kuna umuhimu wa wanachama wa CCM kuchagua Viongozi madhubuti wenye uwezo wa kukivusha chama katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025.

Dk. Mwinyi alieleza kuwepo changamoto mbali mbali zinazokabili chaguzi za chama hicho , ambapo  katika baadhi ya maeneo viongozi wanaogombea hubainika wakiwa wagawaji wa fomu za kupigia kura, jambo ambalo sio sahihi na hivyo akawataka wale wanaotetea nafasi zao kukaa pembeni na kazi hizo kufanywa na wengine.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwapongeza wanachama wa Tawi hilo kwa kufanya uchaguzi kuambatana na  taratibu zinakubalika na kuwataka waendelee hivyo kwenye chaguzi zote zitakazofuatia.

Alisema chaguzi ngazi ya mashina na Matawi ni muhimu katika ustawi wa Chama hicho, kwa kuzingatia ndiko mahala iliko mitaji ya Chama.

Alisema amefarijika kupiga kura katika Tawi hilo la CCM Kilimani na kuwa  mwanachama mpya wa tawi hilo, baada ya kuhamishia makazi yake rasmi Migombani, hivyo akawashukuru wanachama hao kwa kumpokea  na kumkaribisha.

Uchaguzi huo umewashirikisha wajumbe wapatao 182, ambapo jumla ya nafasi sita zinagombewa, ikiwemo ya Mwenyekiti wa CCM  Tawi, Katibu wa CCM Tawi, Katibu wa Siasa na Uenezi, Wajumbe watano wa Mkutano  Mkuu wa CCM Wadi, Wajumbe 10 wa Mkutano Mkuu wa CCM Tawi pamoja na Mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu wa Jimbo na Wilaya.

Wakati huo huo; Dk. Mwinyi alipata fursa ya kusalimiana na kumjuilia hali mwanasiasa mkongwe Asha Simba Mwakwega.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.