Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (wa pili kulia) akiitikia dua iliyoombwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi (wa pili kushoto) leo mara baada ya swala ya Ijumaa liyoswaliwa katika Masjid Sunna Kiwajuni Jijini Zanzibar Mkoa wa Mjini Magharibi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema Serikali itaendelea
kushirikiana na waumini wa madhehebu
mbali mbali ya dini na kusema tofauti ziliopo kati yao haziwezi kuvunja misingi
ya Dini.
Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu alizotoa kwa waumini walioshiriki Ibada ya sala ya Ijumaa, iliofanyika Masjid Sunna, Kikwajuni, Jijini Zanzibar.
Amesema kuna umuhimu wa kuendeleza umoja na amani iliopo, huku akibainisha faida kubwa iliopo kwa waislamu na wananchi kwa ujumla.
Aidha, aliahidi kumalizia maendeleo ya Msikiti huo katika eneo lenye mahitaji, huku akiwashukuru waumini wote waliochangia maendeleo hayo katika maeneo tofauti.
Rais Alhaj Dk.Mwinyi aliwataka waumini hao kuendelea kumuombea Dua ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake na kutimiza yote aliyoyaahidi wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Nae, Kiongozi wa Msikiti huo Sheikh Said ‘Gwiji’ amemshukuru Rais Alhaj Dk. Mwinyi kwa kusimamia vyema uwepo wa amani na umoja nchini, sambamba na mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Kassim Haidar Jabir alisema waislamu wote ni ndugu, hivyo akawataka kuepuka mifarakano, mbali na kuwepo tofauti mbali mbali katika utekelezaji wa Ibada pamoja shughuli za kimaisha.
Alisema pamoja na kufanya ibada mbali mbali, suala la kushikama miongoni mwa waislamu ni jambo la wajibu kwao.
Alisema muumin atakaeshikamana na waumini wengine na kusubiri au kustahamili maudhi ya watu wengine atapata malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Sheikh Said alisisitiza umuhimu wa waislamu kumcha Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza yale aliyoyaamrisha na kuacha yale aliyoyakataza.
Aidha, aliwakumbusha waumini umuhimu wa kuhifadhi neema ya amani na mshikamano uliopo nchini pamoja na kusisitiza haja ya kuwaombea dua viongozi wanaongoza nchini.
Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment