Habari za Punde

Mafanikio zaidi yataendelea kupatikana kutokana na amani, umoja na mshikamo wa wananchi uliopo hivi sasa.


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matarajio yake kwamba mafanikio zaidi yataendelea kupatikana kutokana na amani, umoja na mshikamo wa wananchi uliopo hivi sasa.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo mara baada ya kujumuika pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa huko Masjid Murawwar, Mfikiwa, Mkoa wa Kusini Pemba.

Katika maelezo yake Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba ana imani kubwa baada ya miaka mitano ijayo mafanikio makubwa yatapatikana kutokana na mashirikiano, umoja na mshikamano mkubwa uliopo ambao ameuona wakati wa ziara yake katika mikoa yote ya Unguja na Pemba.

Alhaj Dk. Mwinyi  alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa kuendeleza hatua hiyo ambayo inaleta mwanga wa matumaini na maendeleo makubwa kwa Zanzibar.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa kila mwananchi kuwajibika katika sehemu yake ya kazi ili Zanzibar iweze kupata maendeleo zaidi.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa katika ziara yake yote aliyoifanya Unguja na Pemba amegundua mashirikiano makubwa yaliopo kati ya wananchi sambamba na amani, utulivu na mshikamano uliopo.

Pia, Alhaj Dk. Mwinyi aliipongeza Taasisi ya Milele Foundation kwa juhudi zake za kuiunga mkono Serikali katika kusaidia miradi kadhaa ya maendeleo pamoja na huduma za kijamii.

Aliipongeza taasisi hiyo ambayo imejenga msikiti huo kwa hatua zake za kuendelea kutoa huduma za msikiti huo mpya ambao aliuzinduliwa mnamo Disemba 24, 2021 na Waziri Haroun Ali Suleima kwa niaba ya Alhaj Dk. Mwinyi.

Aidha, Ahaj Dk. Mwinyi amelikubali ombi la kuwa mlezi wa msikiti huo ambao alisifu ujenzi wake ambao unatoa hamu na ari kwa waumini kwenda kufanya ibada wakati wote kutokana na uzuri wake.

Mapema akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Khalifa Mrisho Omar alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Sambamba na hayo, alisisitiza haja kwa walezi na wazazi kuwalea watoto wao vyema na kuwafundisha maadili yaliyo mema.

Nae Meneja wa Milele Foundation Abdullah Said Abdallah alimuhakikishia Alhaj Dk. Mwinyi kwamba taasisi hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi ili kuwasogeze huduma wananchi.

Alieleza kwamba Kamati ya msikiti huo pamoja na waumini wote wa Mfikiwa wataendelea kumuombea dua Alhaj Dk. Mwinyi ili aweze kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano Ikulu,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.