Habari za Punde

Watafiti Watakiwa Kuibua Fursa Uchumi wa Buluu.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei katika mkutano wa Mwaka wa Kisayansi uliofanyika jijini Dar es Salaam Julai 12, 2022.


Na Mbaraka Kambona,

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema watafiti wana nafasi kubwa katika kuendeleza Sekta ya Uvuvi na hivyo wajikite kuibua fursa zinazopatikana kwenye uchumi wa buluu ili ziweze kuvutia wawekezaji wengi na jamii iweze kunufaika.

Aliyasema hayo katika Mkutano wa Mwaka wa Kisayansi uliowakutanisha watafiti mbalimbali wa masuala ya uvuvi uliofanyika jijini Dar es Salaam Jana.

"Dunia kwa sasa inaelekea kwenye uchumi wa buluu, kuhakikisha rasilimali maji zinatumika ipasavyo kwenye kumsaidia mwanadamu na watafiti wana nafasi kubwa sana kwenye jambo hili kwa sababu  kupitia tafiti zao wanaweza kuibua fursa na changamoto zilizopo katika eneo hilo na kuelekeza mbinu na njia za kufanya ili kusaidia Sekta hii ya uvuvi kuwa na mchango mkubwa " alisema

Kufuatia nafasi hiyo waliyonayo watafiti, Naibu Waziri Ulega alisema kuwa watafiti ni muhimu wakatumia taaluma zao kwa kushirikisha jamii inayonufaika na tafiti wanazofanya ili  kuweza kuionesha dunia fursa zilizopo kwenye sekta ya uvuvi kwa lengo la kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Alisema kuwa baharini kuna mazao mbalimbali ambayo yanaweza kusaidia jamii kupata kipato na kuvutia uwekezaji mkubwa.

"Upande wa baharini tuna  Mwani, Majongoo bahari na Kaa, upande wa maziwa tuna  Sato, Sangara na Dagaa, haya yote ni mazao na yakielezwa vizuri na uwekezaji ukapatikana itainua uchumi wa watu wetu," alifafanua

Aliongeza kwa kusema kuwa watafiti wakiibua hizo fursa na kuvutia wawekezaji itakuwa inaenda sambamba na malengo na nia ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kualika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya uvuvi ili kuziamsha kwa maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.

Mkutano huo wa Mwaka wa Kisayansi  unafanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 12 hadi 14 na  umekutanisha watafiti wa masuala ya uvuvi kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana mawazo juu ya namna ya kufanya ili uchumi wa buluu hasa upande wa sekta ya uvuvi kuwa endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.