Habari za Punde

CCM Zanzibar yawataka wananchi kuepuka upotoshaji

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi,akisalimiana na wanachama mara baada ya kuwasili katika maskani ya CCM ya Mjini Kiuyu Pemba.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi,akizungumza na wanachama na mwananchi kwa ujumla katika maskani ya CCM Mjini Kiuyu Wete Pemba katika ziara yake ya kuimarisha Chama.

NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

WANANCHI wameshauriwa kupuuza siasa za chuki na utengano na badala yake waendelee kushikamana kwa kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, katika ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakitoa kauli zisizofaa kwa kubeza hatua za maendeleo zilizofikiwa nchini vitendo vinavyotakiwa kukemewa kabla havijahatarisha amani ya nchi.

Dk.Mabodi alisema CCM imekubali maridhiano ya kisiasa kwa nia ya kudumisha amani,mshikamano na umoja kwa wananchi wote ili serikali itoe huduma bora kwa wananchi bila kujali tofauti zao za kisiasa.

Alisema Chama hicho kitaendelea kuheshimu maridhiano hayo ya kisiasa ambayo yapo Kikatiba huku kikiwahimiza wananchi kuishi kwa upendo na amani kwa maslahi ya ustawi wa maendeleo endelevu.

“Kuna baadhi ya wanasiasa bado hawataki kubadilika wameshikilia historia ya siasa chafu zilizopitwa na wakati, sisi tunaendelea kuwashauri wananchi wawapuuze na kulinda amani iliyopo nchini.

Hivi karibuni tuliwasikia wakibeza miundombinu ya ujenzi wa miradi mbalimbali masoko ya kisasa na majengo ya umma wakidai kuwa nchi imekuwa na ‘’mabati’’ kila sehemu sasa mabati hayo yameanza kuezuliwa na kuonyesha majengo halisi wamekaa kimya.”, alifafanua Dk.Mabodi.

Naibu Katibu Mkuu huyo, aliweka wazi kwamba amani ya Zanzibar imejengwa kwa gharama kubwa hivyo CCM haiwezi kufumbia macho vitendo vya kurejesha nchi katika machafuko.

Alieleza kuwa Chama kimejipanga kushinda kwa zaidi ya asilimia 80 katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Aliwasihi Wana CCM kutumia vizuri fursa ya uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya Chama,kwa kuwachagua viongozi bora na wenye maono,uwezo na uadilifu wa kulinda maslahi ya Chama hicho.

Mapema akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa,alisema Wana CCM katika Mkoa huo wanaunga mkono hatua za kimaendeleo zilizofikiwa na Serikali zote mbili chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia  Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Alieleza kuwa Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa maeneo yanayoneemeka kwa utekelezwaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta za kilimo,miundombinu ya barabara,utalii,uvuvi,afya na elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.