Habari za Punde

Mawakala wa Ajira Binafsi wa Tanzania, Qatar Wajadili Fursa za Ajira

Ujumbe wa Chemba ya Biashara ya Qatar ukizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022

Mawakala wa ajira katika sekta binafsi nchini Tanzania wamekutana na kujadili fursa za ajira na Mawakala wenzao wa ajira binafsi wa Qatar, Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022.

Mawakala hao wameongozana na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Uratibu kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar, Bw. Hamad Ali Elfaifa amesema Qatar na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria ambao umedumu hadi sasa na wanapenda kuuendeleza kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya ajira.

Bw. Elfaifa amewataka Mawakala wa ajira kutoka Tanzania kuzingatia sheria na taratibu za ajira pamoja na kushirikiana na Mawakala wenzao wa Qatar ili kuweza kupata wafanyakazi wenye ujuzi, maarifa na weledi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Vilevile, Bw. Elfaifa ameeleza kuwa katika kutekeleza Mkataba wa Ajira kati ya Tanzania na Qatar, sasa Tanzania imeingizwa kwenye mfumo wa ajira nchini Qatar ambapo mawakala wa Tanzania wataweza kupokea oda za kazi kutoka kwa Mawakala wa Qatar, hatua itakayowezesha watanzania wengi wenye sifa kunufaika na nafasi za kazi nchini Qatar

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania, Prof. Katundu amesema Tanzania inajivunia kuwa na vijana wenye ujuzi na uzoefu katika fani mbalimbali hivyo wanaamini kuwa endapo vijana hao watapatiwa fursa za ajira nchini Qatar watasaidia kuboresha zaidi uchumi wa Qatar pamoja na Maisha yao.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA), Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Joseph Nganga amesema kuwa lengo kubwa la kuwakutanisha mawakala wa ajira binafsi wa Tanzania na wa Qatar ni kufahamishana taratibu za ajira kwa pande zote mbili ili kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano na kupata waajiriwa wenye sifa stahiki.

“Mkutano wa leo umesaidia kufahamu taratibu zinazotakiwa ili kumpata mfanyakazi na stahiki zake hivyo mawakala wa nchi zote watumie fursa hiyo ipasavyo ambapo Mawakala wa Qatar wameonesha kuridhishwa na nidhamu ya vijana wanaoajiriwa kutoka Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na mawakala kutoka Tanzania ili kuwapata wafanyakazi kwenye sekta mbalimbali,” alisema Bw. Nganga.

Mwaka 2014 Tanzania ilisaini mkataba wa makubaliano ya ajira na Qatar, ambapo kwa sasa Serikali ya Tanzania inaangalia namna ya kupata nafasi za ajira kwa Watanzania ili waende kufanya kazi nchini humo.

Ujumbe wa Chemba ya Biashara ya Qatar ukizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022.

Kikao cha Mawawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar kikiendelea Jijini Qatar
Mkuu wa Kitengo cha Uratibu kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar, Bw. Hamad Ali Elfaifa akizungumza na Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar walipokutana Jijini Qatar kujadili fursa za ajira nchini humo
Kamishna wa Kazi, Wizara ya Kazi Zanzibar, Bw. Rashid Khamis Othman akizungumza na Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania na Qatar walipokutana Jijini Qatar kujadili fursa za ajira nchini Qatar
Mmoja kati ya Mawakala wa ajira binafsi kutoka Tanzania akieleza jambo kwa mawakala walioshiriki katika mkutano ulifanyika leo Jijini Doha, Qatar
Mmoja kati ya Mawakala wa ajira binafsi kutoka Qatar akieleza jambo kwa mawakala walioshiriki katika mkutano ulifanyika leo Jijini Doha, Qatar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.