Habari za Punde

Mhe Hemed mgeni rasmi katika Hafla ya Uchangiaji wa Rasilimali za Sensa ya Watu na Makazi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wanajumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar na Wadau mbali mbali katika Kikao cha kuchangia Rasiimali zitakazotumika katika Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kilichofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma akizungumza katika Kikao cha kuchangia Rasilimali zitakazotumika katika Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kilichofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar Ndg.Hamad Hamad akieleza mafupi juu ya Mchango wa Wafanyabiashara na Sekta Binafsi katika Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwka 2022 katika Kikao cha kuchangia Rasilimali ziatakazotumika katika Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kilichofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil
 

Na Abdulrahim Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini Mchango wa Mashirika ya Serikali na Binafsi katika Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa maendeleo ya Zanzibar.

Mhe. Hemed ameeleza hayo katika Hafla ya Uchangiaji wa Rasilimali za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 iliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua umuhimu wa Mashirika hayo kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika Suala la uchangiaji wa Rasilimali za kufanikisha Zoezi hilo.

Mhe. Hemed ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi amesema uhitaji wa Vifaa na Rasilimali Fedha Jumuiya ya Wafanyabiashara, Asasi za Kiraia na Wadau Wengine wamekuwa  Mstari wa mbele kwa kuiunga Mkono Serikali kwa kuleta Mchango mzuri katika utekelezaji wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia Fursa hiyo kuwapongeza Jumuiya ya Wafanyabiashara na Mashirika ya Serikali na Binafsi kwa kuchangia Rasilimali mbali mbali kwa lengo la kufanikisha Utekelezaji wa Zoezi hilo.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lina umuhimu Mkubwa kwa kuiwezesha Serikali na wadau mbali mbali kupata Hisabu halisi ya Idadi ya Watu Nchini pamoja na Taarifa zao za Kijamii, kiuchumi na Makazi yao.

Aidha ameeleza kuwa matokeo yatakayopakana katika Sensa yatasaidia kupata Takwimu Sahihi katika kufanya Maamuzi ya kuleta Maendeleo ya Taifa.

"Takwimu hizi zitasaidia katika kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo wa Muda wa kati wa Zanzibar wa Mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 , ikiwa ni Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050 ambao unalenga katika Uchumi wa Buluu kwa ukuaji Jumuishi na Maendeleo endelevu na Mipango mengine ya Kimataifa "

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amewahakikishia Wadau hao kuwa Rasilimali zitakazokusanywa zitatumika ipasavyo kama ilivyokusudiwa ili kufanikisha Zoezi hilo kwa ufanisi wa Hali ya juu.

Nae Waziri wa Nchi Afisi Ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma ameeleza kuwa Uelewa wa Wananchi kuhusu Sensa ni Mkubwa kutokana na  Uhamasishaji uliofanywa tokea mwanzo wa Mwaka huu hatua ambayo inaashiria kukamilika vyema Zoezi hilo.

Aidha Mhe. Hamza ameeleza kuwa zoezi la Mwaka huu ni la Aina yake ambalo linafanyika kidigitali ambalo litawawepesishia Makazi na Watendaji wa Sensa kuweza kukamilisha Zoezi hilo kwa wepesi zaidi.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndg. Salum Kassim Ali ameeleza kuwa Serikali zote mbili zipo katika Hatua za Mwisho kukamilisha Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka huu ambapo wameona ni vyema kushirikiana na Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi kwa kuchangia Rasilimali zitakazosaidia kukamilisha zoezi hilo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar Ndg. Hamad Hamad ameeleza kufurahishwa kwa kushirikishwa katika Hatua zote za Maandalizi ya Sensa mwaka huu na kueleza kufurahishwa kwao kuona kuwa zoezi hilo kwa Mwaka huu litarahisisha Wananchi kupata Biashara kirahisi kwa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi.

Aidha Ndg. Hamad ameeleza kuwa Sensa hii itasaidia kutoa muongozo Sahihi wa kujua hali za maeneo yanayohitaji uwekezaji hatua ambayo itasaidia Wawekezaji kupata wepesi katika kuelekeza Nguvu zao katika maendeleo ya zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.