Habari za Punde

Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ina Mchango Mkubwa Katika Maendeleo ya Kiuchumi wa Zanzibar - Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza baada ya kumalizika utiaji wa Saini Hati ya Makabidhiano ya "DATA" za Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Vitalu vya Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 10-8-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi wa Zanzibar.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar katika hafla ya Makabidhiano ya Data za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Vitalu vya Zanzibar, kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kupitia Wizara ya Nishati na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Amesema kuna kila dalili zinazoonyesha kuwepo kwa mafuta na gesi asilia hapa nchini hususan katika kitalu cha Pemba - Zanzibar na kubainisha ukubwa wa jambo hilo Duniani katika ukuzaji wa  uchumi pamoja na namna nchi itakavyoweza kubadilika pale mafuta hayo yatakapoanza kuchimbwa.

Dk. Mwinyi aliwataka Wawekezaji wa sekta ya Mafuta na Gesi asilia kuja nchini ili kuendeleza kazi za utafutaji wa nishati hizo na hatimae kuweza kuchimba.

Alitumia fursa hiyo kushukuru mashirikiano makubwa yaliopo kati ya taasisi zinazoshughulikia suala hilo,  Mamlaka ya udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), hususan katika suala la upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Mamlaka ya udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA).   

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ushirikiano uliofanyika ni moja ya maeneo yanayoimarisha zaidi Muungano wa Tanzania na kusema wakati umefika wa kumaliza changamoto chache za Muungano zilizosalia, huku akibainisha na suala hilo limekaaa sawa kisheria na kisiasa. 

Aidha, Dk. Mwinyi alizitaka taasisi zinazoshughulika na uandaaji wa miundombinu ya kuhifadhi Data za utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar kujenga miundombinu hiyo haraka inavyowezekana ili iweze kutumikwa kwa shughuli za uhifadhi.

Dk. Mwinyi aliwashukuru Viongozi waanzilishi wa suala hilo, akiwemo Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  (Awamu ya Saba) Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kazi kubwa na nzuri ya kuliwekea misingi jambo hilo.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa hatua anazochukua kujenga uchumi wa Taifa  kwa  Serikali zote mbili kupitia sekta ya Mafuta na Gesi asilia.

Nae, Waziri wa Nishati wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.January Makamba alisema shughuli za utafutaji wa mafuta zilizokusanywa zimeanzia miaka ya 1950 katika Vitalu namba 9,10,11 na 12 pamoja na Kitalu cha Pemba- Zanzibar.

Alisema tayari Visima 96 vimeshachimbwa ambapo visima 44 vimegundulika kuwa na Gesi asilia kwa wastani Futi za Ujazo 57.4

Alisema makabidhiano na uhamisho wa Data hizo umefanyika kisheria  na kubainisha kuwa ni muhimu kwa sekta ya Mafuta na Gesi  katika kuijengeea uwezo wa kiuchumi Zanzibar.

Alisema kuwepo kwa taarifa hizo kutawahamasisha na kuwavutia watafutaji wa Mafuta na gesi asilia , kwa kigezo kuwa itakuwa ni rahisi kwao kupata pa kuanzia.

Aidha, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame alisema mapokezi hayo ya Data  yamefanyika huku kukiwa na dhamira ya dhati ya serikali katika kufanikisha jambo hilo kwa  vitendo na kutumia fursa hiyo kuwaahidi Wazanzibari kuwa litafanyika kwa umakini mkubwa.

Alisema Data hizo zitakuwa kichocheo kikubwa cha Uwekezaji katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia  na kupongeza mashirkiano makubwa yalioonyeshwa kati ya taasisi zinazoshughulikia suala hilo, hususan katika suala la upatikanaji wa mafunzo na uhifadhi bora wa Data.

Alisema hatua hiyo inaakisi utekelezaji wa vitendo wa miongozo ya Viongozi, sheria pamoja na Katiba za Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya zanzibar.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.