Habari za Punde

Mkutano mkuu wa chama cha madaktari wa watoto Tanzania wafanyika Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa chama cha madaktari wa watoto Tanzania uliofanyika ukumbi wa hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar ambapo amewapongza kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika kukuza sekta ya afya  hasa magonjwa ya watoto nchini.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa madaktari wa magonjwa ya watoto wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.

RAIS wa chama cha madaktari wa magonjwa ya watoto Tanzania Dkt. Pius Muzzazzi akieleza mipango ya chama chao katika hafla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama hicho iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar


Na Abdulrahim Khamis

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefurahishwa na Maamuzi ya Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar katika kuboresha huduma za Afya ya Watoto wachanga.


Rais Dkt. Mwinyi ameeleza hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka 2022 wa Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania uliofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.

Ameeleza kufurahishwa kwa mpango wa NEST 360 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar ambapo Serikali tayari imejipanga katika suala hilo.

Ameeleza kuwa Serikali imejenga Hospitai kumi za Wilaya na Moja ya Mkoa ambapo Ushirikiano Mkubwa unahitajika katika kuwajengea Uwezo Wataalamu ili kutoa huduma ipasavyo katika Hospitali hizo.

Aidha Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kwenye kuboresha huduma za Afya ikiwemo ongezeko la Huduma za Ubobezi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo ameuomba Uongozi wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto kujenga Mfumo wa kusaidia upatikanaji wa Kibingwa bobezi katika Hospitali za Zanzibar hasa katika huduma za Watoto.

Pamoja na hayo Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Zanzibar bado inakabiliwa na vifo vingi vya Watoto walio chini ya Miaka Mitano (05) ambapo nguvu kazi inahitajika zaidi ili kupunguza vifo hivyo na kuwekeza kwenye huduma za Mama na Mtoto kwenye Mifumo ya Afya Nchini.

Pia ameeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza kwa Watoto  yanakuwa Nchini akitolea Mfano Magonjwa ya Moyo,  Magonjwa ya Akili, Saratani, Kisukari na ajali kwa Watoto ambayo huchangiwa na vihatarishi vinavyotokana na Mfumo mbovu wa Maisha.

"Magonjwa haya pia huweza  kuchangiwa na vihatarishi vinavyotokana na Mfumo mbovu wa Maisha, ikiwa pamoja na maisha Bwete (Sedentary Life) hali inayotokana na kupungua michezo ya nje ya Watoto na kukaa katika Luninga na Michezo ya video kwa watoto na kutokuzingatia lishe bora kwa Watoto" amesema

Rais Dkt. Mwinyi amesema Vyama vya Kitaaluma vina Mchango mkubwa katika kuboresha huduma za Afya Nchini ambapo amesisitiza mashirikiano baina yao katika kutoa Elimu, Miongozo, hamasa kwa wanachama wao katika kutoa huduma kwa uadilifu na kuishauri Serikali njia bora za kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wake.

Aidha amekipongeza Chama hicho kwa kusaidia kuleta maendeleo nchini hasa katika kuitangaza fani hiyo pamoja na kuvutia Vijana ili kuboresha utoaji wa huduma za Afya Nchini.

Pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewaomba washiriki wa Mkutano huo kutumia vyema mkusanyiko huo kwa kujadili na kutoa maazimio ya uboreshaji wa huduma za Afya kwa Watoto hasa waliosahauliwa katika Programu za Afya wale wa Miaka mitano hadi kumi (05-10) pamoja na kuweka mipango ya kujenga uwezo kwa watoa huduma za Afya

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar Mhe. HASSAN KHAMIS HAFIDH amesema kuwa kupitia Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania  Wizara itahakikisha inatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kupunguza vifo vya Watoto chini ya miaka mitano (5)

Mhe. HAFIDH amesema kuwa Serikali zote mbili zimefurahishwa  kuona Madaktari Bingwa wa Watoto wa Tanzania nzima wameunda Chama hicho chenye malengo ya kupunguza vifo vya Watoto chini ya Miaka Mitano (5) na kueleza kuwa jambo jema na ni lenye kupigiwa mfano na kuamini kuwa ifikapo mwaka 2030 tanzania itakuwa na idadi ndogo sana ya vifo vya watoto kulinganisha na ilivyo kwa sasa.

Nae Rais wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania (PAT) Dkt. PIUS MUZZAZZI amezipongeza Serikali zote mbili kwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa Huduma za Afya ambapo Watoto ni wanufaika wakubwa wa Huduma hizo na kupanua wigo wa ajira katika sekta ya afya.

Aidha ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kufadhili Madaktari wanaosomea Udakatari Bingwa wa Watoto katika Vyuo mbali mbali na pia kwa Kozi za Udaktari Bobezi wa Watoto, hivyo ameitaka Serikali kuendelea na jitihada hizo za kutoa nafasi zaidi za kusomesha Wataalamu ndani na nje ya Nchi kwani bado Idadi ya Wataalamu hao bado ni ndogo ukilinganisha na mahitaji.

Pia Dkt.MUZZAZZI ameziomba Serikali zote Mbili  kutatua changamoto zinazowakabili Madaktari zikiwemo mpango kazi wa Utumishi wa Umma, Mishahara na nyenginezo ili kuwaongezea ari ya ufanyaji wa kazi Madaktari Bingwa na wale Wataalamu na kuimarisha Huduma za Afya Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kauli mbiu katika Mkutano huo ni MAGONJWA YASIYOKUWA NA KUAMBUKIZA KWA WATOTO - ASIACHWE HATA MTOTO MMOJA.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.