Habari za Punde

JK AMPONGEZA KIJANA MBUNIFU KWA KUTENGENEZA MASHINE YA KUBANGULIA KOROSHO WILAYANI TANDAHIMBA

Rais Mstaafu Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza kijana Zaidu Mbwana kutoka Tandahimba mkoani Mtwara kwa ubunifu wake wa kutengeneza mashine ya kubangulia korosho kwenye alipokutana naye kwenye ofisi za Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) jijini Dar es salaam alikotembelea kijana huyo Jumatato Oktoba 31, 2022.  Wengine ni Afisa Mtendaji Mkuu wa JMKF Vanessa Anyoti na ofisa wa maendeleo ya vijana katika taasisi hiyo, Nicholaus Luoga.

Rais Mstaafu Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza kijana Zaidu Mbwana wa Tandahimba mkoani Mtwara kwa ubunifu wake wa kutengeneza mashine ya kubangulia korosho, na kumtaka auendeleze na kuukuza ubunifu wake huo ili uweze kunufaisha nchi na wananchi maradufu.

Dkt. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF)  ameyasema hayo  Jumatatu Oktoba 31, 2022  alipokutana na Zaidu  kwenye ofisi za taasisi hiyo  jijini Dar es salaam alikotembelea kijana huyo.

Amemshauri kijana huyo kuongeza uzalishaji wa mashine hizo ambazo zimesaidia wakulima wa korosho wa Tandahimba wa kuwa na uwezo wa kubangua korosho hadi magunia mawili kwa siku – kutoka ndoo moja tu.

"Nakupongeza sana kwa ubunifu wako ambao sio tu umesaidia kuongeza tija kwa wakulima wa korosho wilayani Tandahimba bali pia umenufaisha vijana wenzio wengi kwa kujiajiri huku wakiongeza tija kwenye zao la korosho", alisema Dkt. Kikwete. "Sasa angalia namna ya kukuza uzalishaji wa mashine hizo kwa wingi ili izwanufaishe wakulima wa korosho na nchi kwa ujumla..."

Kijana huyo, ambae yuko jijini Dar es salaam kukusanya mali ghafi kwa ajili ya kutengenezea mashine hizo za kubangulia korosho wilayani Tandahimba, alikuwa nyota katika kipindi cha KIJANA LEO  episode ya 6, kinachoandaliwa na JMKF, kwa kushirikiana na AZAM TV Pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. 

Zaidu alifuatwa wilayani kwake Tandahimba na kurekodiwa na baadaye kuoneshwa akionesha ubunifu wake huo kupitia chaneli ya UTV namba 108 kwenye kisimbuzi cha AZAM TV.

Kipindi cha KIJANA LEO ni kipindi cha kipekee kinacholenga kuonyesha jitihada za Vijana wabunifu wanaotatua changamoto mbali mbali katika jamii kwakutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira yao na kutumia fursa hizo kuleta matokeo chanya au manufaa katika jamii zao ikiwemo kutoa ajira kwa Vijana , huduma muhimu na  kufanya kazi kwa ufanisi .

Kijana huyo, ambaye alifurahi na kufarijika sana kukutana ana kwa ana na Dkt. Kikwete, ameishukuru JMKF, AZAM TV Pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa fyrsa ya kujitangaza aliyoipata, na kusema kwamba kipindi cha KIJANA LEO kimemuinua kiuchumi na amekua maarufu nchi nzima kwa namna ambayo hakuitegemea asilani. 

Zaidi ya hayo , Zaidu alifurahi kukutanishwa na wabobezi wa masuala ya biashara na sheria ambao waliweza kumpa mawazo kiundani Zaidi ya jinsi gani anaweza kukuza biashara yake Kwenda masafa marefu katika soko la ndani na nje ya nchi kwenye ofisi za Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) jijini Dar es salaam alikotembelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.