Habari za Punde

Mafunzo ya siku tano kuimarisha ufugaji wa Matango (Majongoo)bahari na kilimo cha mwani yafunguliwa Zanzibar

 Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 07/11/2022.

Mafunzo ya siku tano kwa Nchi Wanachama 15 kutoka Ukanda wa Bahari ya Hindi (IORA) yamefunguliwa Zanzibar ambapo washiriki watapata nafasi ya kujifunza namna bora ya kuimarisha ufugaji wa Matango (Majongoo)bahari na kilimo cha mwani .

Mafunzo hayo yamefanyika hoteli ya Verde mjini Zanzibar na kufunguliwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Sleiman Masoud Makame.

Akifungua mafunzo hayo alisema malengo ya mkutano huo ni kujifunza mbinu bora ya ukuzaji na uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari pamoja na kilimo cha mwani.

Aidha alisema washiriki hao watapata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi wa uzalishaji wa viumbe maji vyenye ubora kwa soko la nchi zao.

Aliongeza kuwa mkutano huo utawapa fursa wanachama hao kutembelea maeneo ya kihistoria ili kupata uelewa  pamoja na kubadilishana uzoefu wa nchi mbali mbali za ukanda wa bahari wa IORA.

Naye Katibu Mkuu wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dk. Aboud Suleiman Jumbe alisema Zanzibar ni moja kati ya nchi tano duniani ambayo inasafirisha kwa wingi mazao ya baharini ambapo kwa mwaka huu tayari imeshavuka lengo iliyojiwekea ya kusafirisha tani 17 za mwani nje ya nchi.

Amesema malengo ya mkutano huo kufanyika Zanzibar inatokana na maendeleo na juhudi za serikali ilizochukua katika kuimarisha mazao ya bahari hasa katika kilimo cha mwani.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agnes R. Kayola amesema nchi wanachama zilizomo katika mwambao wa bahari ya hindi zimekuwa  zikishirikiana katika  mambo mengi ikiwemo masuala ya uchumi wa buluu.

Alifahamisha kuwa kipindi hiki Tanzania iko katika mstari wa mbele kuhakikisha kwamba inazingatia sera iliyopo na kunufaika kwa fursa zote zilizopo nchi wanachama takribani 23 wa IORA zinazoshirikiana pamoja.

Katika Mkutano huo wanachama hao pia watapata nafasi ya kwenda kujionea namna wakulima wa Zanzibar wanavyofanya kilimo cha mwani, matango bahari na mazao mengine ya baharini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.