Habari za Punde

Tanzania na Oman kuongeza ushirikiano

 Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Oman katika kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa  wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mwezi Juni 2022 ili kuimarisha ushirkiano baina ya nchi hizo mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (MB.) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan katika Ofisi za Wizara Zanzibar.

Wakati wa kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine, kilifanyika ili kutathmini utekelezaji wa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wakuu wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mbarouk amesema baadhi ya maeneo tayari yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo maagizo ya kuandaa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2022.

Kadhalika, Balozi Mbarouk ameishukuru Serikali ya Oman kwa kuonesha utayari wa kuanza kuchimba visima 100 vya maji Tanzania Bara pamoja na  kujenga Hospitali katika eneo la Mahonda kwa upande wa Zanzibar ambapo kinachosubiriwa ni mchoro utakaowasilishwa kabla ya kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan amesema Oman imeweka utaratibu wa kuchimba visima 20 kila mwaka ambavyo vitaanza kuchimbwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Kukutana kwa viongozi hao kumelenga kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Oman pamoja na kufuatilia masuala waliyokubaliana wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Oman mwezi Juni 2022.

Pia viongozi hao wamejadili utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa na pande hizo mbili wakati wa ziara hiyo.

Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi za Wizara - Zanzibar

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimfafanua jambo Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan  walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi za Wizara - Zanzibar

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan katika Ofisi za Wizara - Zanzibar

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Oman uliongozwa na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud al Shidhan katika Ofisi za Wizara - Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.