Habari za Punde

Matukio ya udhalilishaji yazidi kuongezeka

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 


Idadi ya matukio ya udhalilishaji katika vitendo vya kubaka na kulawiti yamekuwa yakiongezeka kila mwezi licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa za kupambana na matendo hayo nchini.

Amesema hayo Afisa Takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika Kitengo cha makosa ya Jinai na Jinsia ndugu Ramla Hassan Pandu wakati akiwasilisha ripoti ya matukio hayo ya miezi kumi ya mwaka 2022 wakati wa  mafunzo ya kizazi chenye usawa yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Maisara Mjini Unguja.

Amesema kwa mujibu wa takwimu hizo zinaonesha kuwa Wilaya ya Magharibi B inaongoza kwa kuwa na matukio 207 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ambapo kesi 89 za ubakaji na 31 za kulawiti watoto wadogo waliokuwa na umri  wa miaka 12 hadi mwaka mmoja.

Amesema hali ya matukio ya vutendo hivyo, inasikitikisha sana kwani waathirika wakuu ni watu wenye ulemavu pamoja na watoto wadogo ambao ndio tegemeo kubwa la Taifa la baadae, hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika kupambana na matukio hayo.

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia
Wazee na Watoto, bwana Mohamed Jabir Makame akiwasilisha mada ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasimamia utekelezaji wa mpango kazi wa Kitaifa wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa mwaka 2014 hadi 2022.

Aidha ametaja sababu zinazopelekea kuwepo kwa matendo hayo ikiwemo kuvunjika kwa familia, tamaa na matumizi mabaya ya simu hasa kwa vijana na watoto.

Kwa upande wao washiriki wameishauri Serikali kufuata miongozo ya dini pamoja na kuandaa utaratibu wa kutoa elimu ya jinsia katika ngazi za Shehia, madrasa, pamoja na Skuli ili kutokomeza matendo hayo.

Pia wamesema kufanyiwe marekebisho ya sheria ya mtoto ya mwaka 2011, katika kipengele cha adhabu kwa kushushwa umri wa kupewa adhabu kwa watoto, kwani imeonekana nao wamekuwa wakifanyiana wenyewe kwa wenyewe.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewashirikisha viongozi wa dini, maafisa Ustawi, maafisa waratibu wanawake na watoto wa Wilaya, watu wenye ulemavu, masheha, asasi za kiraia pamoja na vijana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.