Habari za Punde

Mhe Othman akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Msoud Othman, ameiyomba Serikali ya Japan kuangalia uwezekano wa kupanua wigo wake wa ushirikiano  na Zanzibar katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia  nchi hasa katika maneo ya fukwe  zinazoharibika kwenye maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko Ofisini kwake Miogombani mjini Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Japan nchi Tanzania Bw. Misawa Yusushi  kwa mazungumzo rasmi yanayohusu ushirikiano kati ya nchi hiyo na Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Mhe. Makamu amesema kwamba kutokana na athari ya mabadiliko ya Tabia nchi inayoendelea, yapo maeneo kadhaa katika visiwa vya Unguja na Pemba,yakiwemo ya kilimoi na mkaazi ya watu kama vile Nungwi, Jambiani na Tovuni maji ya bahari tayari yanaendelea kusogea  jambo ambalo  linaloleta athari kwa jamii.

Amefahamisha kwamba suala la mabadiliko ya tabia nchi tayari limesababisha athari kubwa ya kimazingira  na kuonekana kuwa ni tishio kubwa kwa wananchi wa Zanzibar hasa maeneo ya makaazi ya watu napovamiwa na maji ya chumvi na kuathri shughuli nyengine za kijamii na kilimo.

Mhe. Makamu amesema pamoja na jitihada za serikali  katika kukabiliana na hali hiyo kupitia uhifadhi wa mazingira, lakini suala hilo linahitaji uwezo mkubwa wa kiufundi, kitaalamu na kifedha katika kukabiliana nalo na kwamba ni vyema serikali hiyo kuangalia maeneo zaidi katika kuisaidia Zanzibar.

Aidha aliyataja maeneo mengine yaliyo chini ya Ofisi yake ambayo ni muhimu kuwepo na kuzidisha wigo wa ushirikiano wa namna hiyo ni pamoja na suala la mazingira, mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na  masuala ya udhailishaji.

Amesema kwamba Zanzibar inathamini na kuridhishwa sana na ushirikiano uliopo kati yake na Japan kupitia miradi mbali mbali ya maendeleo ya Zanzibar ikiwemo sekta ya uchumi wa bluu na uvuvi inayotekelezwa kwa pamoja na serikali ya Zanzibar na nchi hiyo.

Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Misawa Yusushi, amesema kwamba nchi yake inaoushirikiano wa muda mrefu kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar na kwamba itaendelea na jitihada hizo ili kuisaidia Zanzibar katika maeneo tofauti.

Amefahamisha kwamba Zanzibar inazo fursa nyingi za Ushirikiano kati yake na Japan na kwamba itaendelea kuangalia maeneo zaidi katika kuendeleza mashirikianio hayo hasa kwa vile nchi yake nayo ni ya visiwa kama Zanzibar.

 


Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo tarehe 10.01.2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.