Habari za Punde

Naibu Katibu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Ndg.Shomari Apongeza Jitihada za Viongozi Wakuu Katika Kuimarisha Mawasiliano Nchini

Naibu katibu Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi  Zanzibar Ndugu Shomari Omar Shomari amepongeza jitihada zinazochukuliwa na viongozi wa kuu wa Nchi katika uimarishaji wa huduma za Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari.

Naibu katibu Mkuu Shomari ameeleza hayo wakati akikifungua kikao kazi kilichowashirikisha wadau mbalimbali kutoka katika Wizara na Taasisi za Serikali kilichotoa maoni yatakayowezesha kupata taarifa za ufanikishaji wa upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhi bidhaa za biashara mtandao.

Amesema kikao hicho ni matokeo ya ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi Nchini Oman ambapo wameoneshwa kuvutiwa kwao na huduma zinazotolewa na Shirika la Posta la Oman (ASYAD) kutokana na mifano wanayotumia katika kufanya biashara mtandao.

Naibu katibu Shomari amefafanua kwamba utekelezaji huo wa uimarishaji wa huduma za teknolojia ya Habari na Mawasiliano unakwenda sambamba na mpango wa dira ya Maendeleo ya Serikali  2050 pamoja na ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 – 2025.

Wakizungumza mara baada ya kikao hicho Mkurugenzi wa idara ya Mawasiliano na Mkurugenzi wa Jackson Group Kelvin Twissa wamesema mpango huo utakapo kamilika utaiwezesha Nchi kufungua fursa zaidi kwa wananchi wake kwa kufanya biashara kwa kutumia njia ya mtandao sambamba na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali.

Wakurugenzi hao wameeleza kuwa Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwa kutumia miundombinu yake katika kusambaza bidhaa zake kwa nchi zilizo katika ukanda wan chi za Sahara.

Aidha wamefafanua kwamba ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa hapa Nchini utaongeza wigo kwa Taasisi za ukusanyaji wa Mapato  kukusanya zaidi kutokana na kampuni nyingi kupitisha bidhaa zake Tanzania.

Wadau kutoka taasisi mbalimbali wameshiriki  katika kikao hicho kwa ajili ya kutoa taarifa zitakazo wezesha kufanikisha kazi hiyo ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za biashara mtandao Tanzania.

Taasisi hizo zina jumuisha Shirika la Bandari Zanzibar, ZICTIA, ZMA, KILIMO,  BIASHARA, ZRA, Pamoja na wadau wengine.

Imetolewa na kitengo cha Habari (WUMU)

Januari 16, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.