RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya
mazoezi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yasioambukiza ukiwemo ugonjwa wa
moyo.
Alisema hatua
hiyo imethibitishwa na wataalamu wa
afya kupitia utafiti walioufanya unaoonesha moja ya hatua muhimu ya kukabiliana
na magonjwa hayo ni kufanya mazoezi.
“Nawasihi nyote muendelee kushiriki
kwenye kambi mbalimbali za upimaji wa magonjwa na matembezi kama haya, kwani ni
muhimu kwa afya zenu, kila mtu huko anakoishi atambue kufanya mazoezi ni kinga
muhimu katika kuepuka magonjwa mengi hasa yasio ambukiza, kwa hiyo sote
tuhimizane tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi na kupima afya zetu mara kwa
mara ili kubaini mapema kama tuna matatizo ya kiafya, kuchukue hatua za
matibabu” Alishauri Dk. Mwinyi.
Rais Dk.
Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya Amani, Zanzibar alipofunga kambi na kampeni
za upimaji na tembea na taasisi ya moyo
Jakaya Kikwete (JKCI).
Alisema taifa
linatumia pesa nyingi
za kigeni kugharamia matibabu ya moyo na magonjwa mengine nje ya nchi. Hivyo
aliipongeza taasisi ya JKCI kwa kubunifu mikakati mbali mbali ya kinga na tiba
ya maradhi ya moyo nchini.
Aidha, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwajengea
uwezo watumishi wa afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwasihi
kuendeleza utamaduni huko kwa watumishi wa Pemba.
“Nawasihi JKCI mfike na Pemba kwa ajili
ya uchunguzi na kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kama njia bora ya kuimarisha
afya, bila ya shaka wananchi wa Pemba nao wanahitaji huduma zenu na elimu hii
kama mlivyofanya hapa Unguja” Alishauri Dk. Mwinyi.
Katika
hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi aliitaka
taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete kuongeza huduma zao kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na kueleza
kuwa kuwepo kwao kutasaidia kupambana na matatizo mbali mbali ya afya ambayo
jamii wanakabiliana nayo.
Alieleza hatua hiyo itasaidia kuongeza
uwezo na wataalamu watakao wahudumia vizuri wananchi na kupunguza madhara ya
magonjwa haya ambayo yanaongezeka kila siku.
Alisema tokea kuanzishwa kwa taasisi
hiyo, mwaka 2015 tayari imesaidia wagonjwa wengi wakiwemo waliotibiwa kwa dawa
na waliofanyiwa upasuaji na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyoa aliitaka
taasisi hiyo kuimarisha utendaji wao na kuongeza tija kwa watu wengi kunufaika
na huduma zao.
“Nafahamu kuwa taasisi hii imekuwa na
utendaji mzuri sana tokea ilipoanzishwa. Hata hivyo, bado kuna nafasi ya
kufanya vizuri zaidi ili kuyafikia malengo ambayo Tanzania tumejiwekea, katika
kuimarisha afya za wananchi kwa kutoa huduma bora na zenye kiwango cha
kimataifa”. Alieleza.
Akizungumza kwenya hafla hiyo, Waziri wa
Afya, Nassor Mazurui alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watashirikiana
na taasisi ya JKCI, kuongeza wataalam wa matatizo ya moyo Zanzibar kutokana na
uhaba wa wataalamu hao ambapo alieleza kwasasa wapo wawili tuu.
Alisema alisema Zanzibar kwa sasa ina
madaktari bingwa wawili tuu wanaoshughulikia matatizo ya moyo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.
Peter Richard Kisenge, alisema taasisi yao kwa kushirikiana na Wizara ya Afya
Zanzibar, kupitia hospitali kuu ya Mnazi Mmoja wataendeleza matibabu ya moyo
kwa kutoa huduma za kuvimba kwa moyo na upasuaji mkubwa wa moyo kwa wananchi ili
kudumisha ushirikiano wao kwa vitendo.
Alisema kampeni walioidanya wiki nzima Unguja alieleza walifanikiwa
huwahudumia wagonjwa 718, wakubwa 627 na watoto 91 ambao walifanyiwa vipimo vya
matibabu ya moyo, sukari na magonjwa mengine.
Dk. Kisenge aliongeza kati ya watu wazima 627 waliopimwa matatizo ya
moyo, 549 waligunduliwa wana ugonjwa wa moyo alieleza katika hatua hiyo walitoa
vifaa 75 kwa baadhi ya wagonjwa na kueleza kuwa 46 walipewa watu wazima na
vifaa 29 walipewa watoto.
Kampeni ya upimaji ya magonjwa yasiyoambukiza ya (JKCI) iliadhimishwa
kwa kauli mbiu yao “TEMBEA NA
TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) na WIZARA YA AFYA, LINDA AFYA YA MOYO
WAKO”
IMETAYARISHWA NA DARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment