RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru
Serikali ya Sweden kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kuisaidia kwenye masuala mbalimbali ya uchumi na Maendeleo.
Dk. Mwinyi alitoa shukurani hizo Ikulu, Zanzibar
alipozungumza na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, bi. Charlota Ozaki Macias.
Alisema hatua ya Serikali ya Sweden kuisaidia
Zanzibar kwenye sekta za Elimu na kilimo cha baharini, ikiwemo kilimo cha mwani
na kuwasaidia kinamama kisiwani Pemba kwenye kilimo cha ufugaji Samaki ni
kuendeleza jitihada za Serikali ya awamu ya nane katika kutekeleza adhma yake
ya kuongeza ajira kwa wananchi wake hasa kuwainua wananwake kiuchumi.
Dk. Mwinyi aliiomba Serikali ya Sweden kupitia
balozi wake huyo kuisaidia Zanzibar kwenye Sekta ya Nishati, alisema Zanzibar
inadhamira ya kuzalisha umeme wake hivyo, iko tayari kwajili ya mazungumzo na
kampuni yoyote kutoka Sweden ili waanze hatua za upembuzi yakinifu na kueleza
kwamba Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO) liko tayari kwa hatua hiyo kuanza
wakati wowote.
Alisema ni jambo la faraja endapo Zanzibar
ikipata kujitegemea kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme, Dk. Mwinyi
alimueleza balozi huyo, kwamba Zanzibar inapokea megawatt 100 tuu ambao pia
inapata msaada kutoka Tanzania Bara.
Kuhusu dhamira yake ya kuimarisha Uchumi wa Buluu
Visiwani, Rais Dk. Mwinyi aliishukuru serikali ya Sweden kwa hatua yake
yakuendeleza jitihada zao kwenye sekta hiyo pia alimueleza balozi huyo kwamba
miradi wanayoiendeleza kwa wakulima wa mwani na wafugaji samaki kisiwani Pemba,
ni hatua ya Serikali kuwainua wananchi kwa kuwawezesha kimaendeleo.
Alisema ukulima wa mwani kwa Zanzibar ni shughuli
inayofanywa na kina mama wengi hivyo, aliipongeza Serikali ya Sweden kwa kuwawezesha
wanawake hao.
Kuhusu sekta ya Elimu rais Dk. Mwinyi alimueleza
mgeni wake huyo kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikisha miradi
mingi ya maendeleo kwenye sekta hiyo na kueleza kwamba bado inahitaji kuungwa
mkono kwenye sekta hiyo.
Naye, Balozi wa Sweden nchini
Tanzania bi. Charlota Ozaki Macias, alimueleza Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Sweden
inafanyakazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar ambayo
alieleza wanashikiriana kwenye Masuala mbalimbali ya maendeleo.
Balozi Charlota alisema wameshirikiana na Wizraya
ya Elimu na Mafunzo ya Amali walifanikisha mradi mbalimbali ikiwemo mradi wa
kuwapa mafunzo ya vitendo na kuwawezesha vijana na wasichana wengi walioacha skuli
kwa kuwafungua kitaaluma na vitendo.
Alisema Serikali yake itashirikiana na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua tatizo la umeme nakueleza kwamba nchi
yake inawataalamu wakutosha kwenye masuala ya nishati.
Aidha, alimuahidi Rais Mwinyi kwamba Serikali ya
Sweden na Zanzibar wataendeleza ushirikiano uliopo katika kukuza Sekta ya
uwekezaji na kumuahidi kwamba wapotayari kwa hatua za upembuzi yakinifu kwenye
masuala ya uwekezaji.
Uhusiano wa Diplomasia baina ya Tanzania na
Sweden umeanza miaka 50 iliyopita kwa mataifa hayo mawili, kushirikina kwenye
masuala mbalimbali ya maendeleo, jamii na uchumi kupitia shirika lake la Sida, Sweden
imeisaidia sana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwenye sekta ya elimu hasa
kwenye ujenzi wa skuli, kuongeza vyumba vya madara pamoja na rasilima nyengine
za elimu.
Tanzania ina ubalozi wake nchini humo kwenye mji mkuu
wa nchi hiyo, Stockholm ambapo Balozi, Grace Alfred Olotu ni Balozi wa Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa nchi za Nordic, mataifa ya Baltik na Ukraine.
Nchi ya Sweden yenye mji mkuu wake Stockholm, iko kaskazini mwa bara Ulaya katika
penensula ya Scandnavia, inapakana na nchi za Norway kwa upande wa Magharibi na
Kaskazini, inakaribiana na nchi ya Finland kwa upande wa Mashariki na Kusini
Magharibi iko karibu na Denkmark.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment