Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kutoa Taarifa Mapema za Viashiria vya Uhalifu Badala ya Kuliachia Jeshi la Polisi Kupambana na Matendo Hayo

 

Wakili wa Serikali mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga, akizungumza katika halfa ya kutoa elimu ya Sheria kwa wananchi wa Fuoni ikiwa ni shamra shamra za kuadhimisha Wiki ya sheria Zanzibar. Kulia ni Wakili wa Serikali kutoka afisi ya Mwanasheria Mkuu Mbarouk Suleiman Othman na kushoto ni Sheha wa Uwandani Juma Mussa Juma

Jukumu la kuzuia vitendo vya kihalifu na maovu katika jamii linapaswa kufanywa na kila mtu katika eneo lake badala ya kuliachia Jeshi la Polisi peke yake kama watu wengi wanavyofanya.

Hivyo wananchi katika mitaa yao wanawajibika kutoa taarifa ya viashiria au matendo ya kihalifu kwa Jeshi hilo au viongozi wa Shehia ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa Serikali mwandamizi kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga, aliyasema hayo huko Fuoni Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akiwasilisha mada katika ziara za kutoa elimu ya kisheria kwa jamii (outreach program) ikiwa ni mwendelezo wa shamra shamra za Wiki ya Sheria Zanzibar ambayo kilele chake ni Februari 13, mwaka huu.

Amesema kushamiri kwa maovu katika jamii kama vile biashara na matumizi ya Madawa ya kulevya, udhalilishaji au migogoro ya ardhi huchangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya muhali iliyojengeka kwa watu wengi na hivyo kushindwa kuwafichua watendaji wa maovu katika jamii.

Amesema ni vyema pale inapotokea ishara tu ya jambo ovu lolote wananchi wanapaswa kutoa taarifa badala ya kukaa kimya kwa kuogopa kuonekana mbaya na watendaji wa makosa hayo.

“Chukulia mfano mtaani kwenu wamekuja watu wasioeleweka, wakaanza kuvuta Bangi au madawa yoyote, wewe ukakaa kimya, au mwanafamilia ametenda kosa ukaendelea kukaa kimya, tambua kuwa unatengeneza mazingira ya kufanyika makosa zaidi. Ikiwa utaenda kupeleka Taarifa kwa Sheha au Polisi itakuwa umesaidia kuiepusha jamii kuharibika dhidi ya makosa ambayo yangefanywa zaidi na muhusika.” amesema Wakili Hamisa.

Hata hivyo, wanachi wengi waliohudhuria katika Mkutano huo walikuwa na shauku ya kusikia hatua zinazochukuliwa kupambana na Madawa ya kulevya pamoja na matendo ya udhalilishaji ambayo yanawakosesha amani wakaazi wa Fuoni.

Mmoja wa wakaazi hao wa Fuoni Bi Salma Ali alitaka kujua sababu zinazopelekea kukamatwa wasambazaji na watumiaji Madawa ya kulevya kuwa ni vijana wadogo masikini, wakati wafanyabiashara wakubwa wa Madawa ya kulevya wanafahamika bila kuchukuliwa hatua.

Amesema wananchi wengi wana hamu ya kuona wafanyabiashara wakubwa wa Madawa ya kulevya wanaotoa dawa hizo nje ya nchi wakitiwa hatiani na kupewa adhabu, badala ya kila siku kuonekana vijana wadogo watumiaji peke yao ndio wanaotiwa hatiani.

“Kila siku tunaona na kusikia wanaokamatwa ni watoto wetu wadogo wanaotumia Unga lakini hayo Mapapa yanayofanya biashara na kutuletea hapa hatuyaoni kufungwa wala kukamatwa, na yanajulikana mambo haya vipi” aliuliza Bi Salma.

Akijibu swali hilo Wakili kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Issa Ahmed amesema hakuna Taarifa ya wafanyabiashara hao wakubwa wanaodaiwa kufanya biashara hiyo.

Ameongeza kuwa kma kuna mwananchi yeyote mwenye taarifa ya wafanyabiashara Wakubwa na wadogo anapaswa kulijulisha Jeshi la Polisi ili lifanye kazi yake.

“Sisi tunataka hao wanaojulikana Mapapa wa Madawa ya kulevya waripotiwe katika Jeshi la Polisi. Uzuri zaidi ni kwamba Jeshi linatunza siri ya mtoa taarifa. Wala mwananchi aliyetoa taarifa hiyo hatoitwa mahakamani” Alifafanua Wakili Issa.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Mrakibu wa Polisi Fuoni Denis Tumbo amesema Jeshi la polisi lipo tayari muda wote na hivyo aliwashauri wananchi hao kuwa karibu na Jeshi hilo ili kufanyakazi ya kulinda usalama wa wananchi wote.

Katika kuonesha ushirikiano thabiti wametoa namba za simu kwa wananchi hao kuwapigia muda wote kunapokuwa na tukio au viashiria vyovyote vya uhalifu kama Madawa ya kulevya, udhalilishaji au hata migogoro ambayo huleta tafrani katika jamii.

Ziara hiyo iliyoandaliwa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa kushirikiana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ilikuwa na lengo la kuwafahamisha wananchi sheria kama njia moja wapo ya kusaidia kupunguza migogoro ikiwemo ya Ardhi, vitendo vya udhalilishaji, madawa ya kulevya na uhalifu katika jamii.

Wiki ya Sheria mwaka huu imeanza Febuari 6 na kilele chake kinatarajiwa kuwa Febuari 13, ambapo Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar katika kuadhimisha siku hiyo wamefanya ziara za kutoa elimu ili kuisaidia jamii kuwa na ufahamu wa maswala ya kisheria jambo litakalosaidia kupunguza migogoro na uhalifu nchini.

Wakili kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Issa Ahmed akiwasilisha mada ya athari ya Madawa ya kulevya katika shamra shamra za wiki ya sheria Zanzibar huko Fuoni, mjini Unguja.
Mrakibu wa Polisi Fuoni ASP Denis Tumbo akitoa nasaha zake za kuwataka wanajamii ya Fuoni kutoa mashirikiano kikamilifu ili kupunguza vitendo vya kihalifu.
Mratibu wa Wanawake na Watoto shehia ya Fuoni Uwandani Husna John akichangia katika halfa ya utolewaji wa elimu ya sheria kwa wananchi wa Fuoni iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kushirikiana na DPP ili kupunguza vitendo vya kihalifu Zanzibar.
Masoud Siasa Masoud kutoka Fuoni akiuliza kuhusu hatua zinazochukuliwa kupunguza uingizwaji wa madawa ya kulevya nchini katika hafla ya utolewaji wa elimu ya Sheria iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar na DPP.   

Wanafunzi na wazee wakifuatilia mada zilizotolewa na Mawakili wa Serikali huko katika kijiji cha Matemwe, ikiwa ni shamra shamra ya wiki ya Sheria Zanzibar.

Wanafunzi na wazee wakifuatilia mada zilizotolewa na Mawakili wa Serikali huko katika kijiji cha Matemwe, ikiwa ni shamra shamra ya wiki ya Sheria Zanzibar.

                  Picha na Faki Mjaka-Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.