Habari za Punde

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe.Simai Mohammed Said Akiwa Ziarani Nchini Oman

 

Muscat - Oman 13-02-2023
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar Mheshimiwa Simai Mohammed Said akiambata na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe na Mkurugenzi wa Makumbusho na Mambo ya Kale wapo ziarani nchini Oman kwa lengo la kukuza uhusiano baina ya Zanzibar na Oman huku nchi mbili hizi kufikia muafaka wa uwekaji saini baina ya Serikali ya Oman na Kampuni Nandhra Engineering and Construction Company Limited ya Tanzania kwa ajili ya kuanza ukarabati mkubwa wa Jengo la Makumbusho la Bait Al Ajaib.
Ujenzi huu ambao utagharimu kiasi cha Dola za Kimarekani Millioni 21 (21Mil US$, takribani Shilingi Bilioni 50) unatakiwa matayarisho yake kuanza mwezi huu February 2023 na Mkandarasi anatakiwa kuanza rasmi ujenzi wake ndani ya miezi mitatu ijayo na unatakiwa ukamilike ndani ya muda wa miaka mitatu.

Katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mheshimiwa Simai ameeleza kwamba ujenzi huo unatarajiwa kuanza mapema ndani ya miezi mitatu mara tu ya utiaji saini wa mkataba huo na fedha hizo zitatumika katika kutayarisha mambo yanayohitajika kuufanikisha ujenzi huo.

Jengo hilo la kihistoria linatarajia kuwa na Makumbusho kubwa ya kisasa kwa ajili ya kuihifadhi na kuitangaza historia ya Zanzibar kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.

Aidha, Mhe.Simai amesema, utiaji saini wa Mkataba huo kutapelekea kuzileta nchi mbili hizi karibu zaidi pamoja na kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo, huku akiongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale itaendelea kushirikiana na Serikali ya Oman katika kuliendeleza na kulisimamia Jengo hilo ambalo ni urithi Mkubwa na mashuhuri Barani Afrika.
Ujumbe wa waziri wa Utalii na mambo ya Kale wa Zanzibar Mheshimiwa Simai Mohammed Simai unatajiwa kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ya makumbusho na ngome za Kihistoria kama vile Ngome kongwe ya Nizwa (Nizwa Fort), Makumbusho ya Taifa ya Oman na Royal Opera House ikiwa ni sehemu ya kujionoea na kujifunza uhifadhi wa historia ya nchi zetu.

Itakumbukwa kuwa Jengo la kihistoria la Bait Al-Ajaib lilijengwa na Mfalme wa pili wa Zanzibar Sultan Barghash Bin Said hapo mwaka 1883 na mnamo Disemba mwaka 2020 jengo hilo liliporomoka sehemu kubwa na kulazimika kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Jengo la Bait Al Ajaib ni moja ya sehemu muhimu ya Hifadhi ya Mji mkongwe unatambulika kimataifa na Jumuiya ya UNESCO.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.