Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdullah Atembelea Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Munduli.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwasalimia wafanyabiashara wa soko la Munduli alipowasalimia wakati akimaliza ziarra ya kukagua ujenzi wa skuli ya Munduli ambapo amewahakikishia kuwa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi itapanga utaratibu wa kuweka mnadi katika soko hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemtaka Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar kusimamia  mkataba wa ujenzi wa Skuli ya Munduli ili ikamilike kwa wakati.

Mhe. Hemed ametoa kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa Skuli ya Munduli Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ inayojengwa kwa fedha za ahueni ya Uviko 19.

Amesema ni Imani ya Serikali kuwa mkandarasi huyo atasimamia ujenzi huo kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kukamilisha mradi huo kwa kiwango na kwa wakati uliopangwa.

Amesema Serikali ina wajibu wa kujenga Miundombinu imara na ya kisasa inayoendana na wakati hali ambayo itapelekea upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar.

Akigusia kuhusu suala la fedha za mradi huo Mhe. Hemed amesema Serikali tayari ilishatenga fedha kwa ajili ya mradi huo. Hivyo,  ameutaka Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha fedha hizo analipwa mkandarasi kwa mujibu wa utaratibu uliopo ili aweze kukamilisha ujenzi kwa wakati.

Sambamba na hayo Makamu wa Pilli wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa ujenzi huo kwani ujenzi huo utakapokamilika watakaofaidika zaidi ni watu wa maeneo hayo na maeneo ya jirani.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa kukamilika kwa Skuli hiyo kutaweza kuwasaidia Walimu kufundisha katika mazingira mazuri ya kusomeshea na kujifunzia jambo ambalo litaongeza ufaulu wa wanafunzi hapa nchini.  

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekipongeza Chuo cha Mafunzo Zanzibar  kwa hatua nzuri waliofikia katika ujenzi wa Skuli hio na kuwasihi kusimamia mkataba ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachokubalika kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa ameeleza kuwa Wizara inaendelea kusimamia maendeleo ya ujenzi huo na kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa kiwango kinachokubalika.

Kwa upande wake Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis amemuhakikishia Mhe. Hemed Kuwa  ujenzi unaendelea vyema chini ya ukandarasi wa Chuo hicho na kuahidi majengo ya Skuli ya Munduli kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesimama kuwasalimia wafanyabiashara wa soko la Munduli na kuwaeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Mwinyi inawathamini Wananchi wake wakiwemo wafanyabiashara wadogo wadogo

Aidha Mhe. hemed ameeleza kuwa atakaa na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi ili kulifanyia kazi ombi la wafanyabishara hao la uwepo mnada katika soko hilo kwa lengo la kukuza biashara zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.