Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip
Mpango leo tarehe 23 Machi 2023 akikagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha
Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip
Mpango leo tarehe 23 Machi 2023 ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya
maendeleo inaotekelezwa katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa barabara ya Buhigwe - Muyama – Kasumo.
Amesema barabara hiyo ni jitihada za serikali katika kuufungua mkoa wa Kigoma
na kuunganisha na mikoa mingine pamoja na nchi jirani hivyo kuchochea biashara
na ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Amewataka viongozi wa chama na serikali katika mkoa huo kuwa na
ushirikiano ili kufanikisha miradi kwa haraka zaidi na kwa ufanisi. Makamu wa
Rais amewataka wananchi kutambua gharama za maendeleo ni pamoja na kujitoa
hivyo wanapaswa kuunga mkono tathimini na fidia zitakazotolewa na serikali
kupisha ujenzi wa mradi huo.
Halikadhalika Makamu wa Rais
amekagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo na nyumba za wahudumu wa afya
wa zahanati hiyo,mradi unaotekelezwa kwa
nguvu za wananchi kwa kushirikiana na serikali. Amewapongeza wananchi wa Kijiji
hicho kwa kujitolea kuongeza eneo la zahanati hiyo pamoja na kutoa mchango wa
hali na mali katika utekelezaji wa mradi huo na kuwaasa kuendelea kutoa mchango
wao katika miradi mingine.
Makamu wa Rais amesema serikali itafanya ukarabati wa nyumba za walimu
katika shule ya msingi Lemba iliopo jirani na zahanati hiyo ambayo inakabiliwa
na changamoto ya uchakavu kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa shule mpya ya
sekondari ya wasichana kidato cha tano na sita yenye jumla ya majengo 18
inayojengwa katika kata ya kajana Kijiji cha kasumo. Pia amekagua ujenzi wa
jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wilaya ya Buhigwe, Mradi wa Ujenzi wa Ofisi za Chama cha Mapinduzi Wilaya ya
Buhigwe pamoja na Ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
Makamu wa Rais amewasihi wakandarasi kuendelea kutoa fursa kwa wazawa wa
maeneo husika ya ujenzi ili waweze kujiinua kiuchumi. Pia amewataka wananchi wa
wilaya ya Buhigwe kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutumia vema fursa za miradi iliopo
wilayani humo kujipatia maendeleo.
Pia Makamu wa Rais amewataka wananchi hao kutoa kipaumbele katika elimu
kwa kutumia vema fursa iliotolewa na serikali ya awamu ya sita kutoa elimu bila
malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.
No comments:
Post a Comment