Habari za Punde

Filamu za Historia ya Nchi Kuandaliwa

Na Shamimu Nyaki

Serikali kupitia Bodi ya Filamu inaratibu mpango mahususi wa uandaaji wa filamu zinazohusu maisha ya viongozi na historia ya nchi ikiwemo maisha ya Baba wa Taifa Hayati  Mwalimu Julius Nyerere.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma Aprili 28,2023 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa anajibu swali la Mhe. Mussa Omar Salim (Gando)  lililoulizwa kwa niaba yake na Mhe. Kassim Hassan Haji (Mwanakwerekwe)  aliyeuliza mkakati wa Serikali katika kuandaa Filamu zinazoelezea historia ya nchi.

"Kwa sasa Bodi ya Filamu kwa kushirikiana na wadau wa filamu inaratibu mpango wa kuandaa filamu itakayoelezea maisha ya Bibi Titi Mohamed, Chifu Kingalu na Mtemi Mirambo" amesema Mhe. Mwinjuma.

Ameongeza kuwa, mwaka 2021 kupitia mwaandaji wa filamu Adam Juma aliandaa Filamu iliyoelezea ushujaa wa viongozi wetu katika kupambania nchi, ambapo  mwaka 2022 kupitia studio ya Wanene iliandaa makala maalum inayotangaza mandhari ya kupiga picha za Filamu nchini, huku akiongeza kuwa Mkataba uliosainiwa hivi karibuni kati ya Bodi ya Filamu na Taasisi ya BUSAN kutoka Korea Kusini utasaidia utengenezaji wa filamu bora zaidi.

Aidha, Mhe. Mwinjuma alijibu swali la nyongeza la Mhe. Fransic Mtinga (Iramba Mashariki) lililohusu mgawanyo wa mapato katika uwanja wa  Mkapa Dar es Salaam na kueleza  kuwa, mapato hayo hugawanywa  kulingana na taratibu zilizowekwa ambazo zimezingatia utunzaji, uendeshaji pamoja gharama za mchezo husika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.