Muonekano wa baadhi ya Nyumba 124 na Misikiti miwili na vitu mbalimbali vya vilivyoathirika na upepo mkali uliotokea mwanzo mwa mwezi huu wa Aprili katika Shehia Sita Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi mati 80 kwa ajili ya Ujenzi wa Msikiti msikiti ulioathirika na upepo katika Shehia ya Kigongoni na kupokea mabati 50 yaliyotolewa na Bw. Makame Simai. (kulia kwake) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na kuwafariji Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walipota athari za upepo uliotokea hivi karibuni na kuharibi makazi yao na vipando katika mashama yao.
Na.Abdulrahim Khamis. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezifariji Familia zilizoathirika na upepo uliotokea Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Jumla ya nyumba Mia Moja Ishirini na Nne (124) na Misikiti Miwili (02) miti na vipando vimeathirika kutokana na upepo mkali uliotokea Aprili Mosi na Aprili Saba mwaka huu katika Shehia sita za Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akiwafariji wananchi hao Mhe. Hemed ameeleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anaungana nao na anawaombea kwa M/ Mungu Mtukufu wawe na Subra katika kipindi hichi cha Mtihan huo.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikishirikiana na wadau mbali mbali watahakikisha wananchi hao wanarudi katika makazi yao ya awali ndani ya kipindi kifupi.
Aidha Mhe. Hemed amewapongeza wananchi waliowahifadhi waathirika hao katika makazi na kueleza kuwa kitendo hicho kinaonesha umoja na mshikamano katika jamii.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefarijika kuona wananchi hao licha ya Mtihani huo walioupata wameupokea kwa kadari yake Allah na bado wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi ikiwemo, kilimo, Uvuvi, ufugaji na biashara.
Mhe. Hemed amewashukuru wadau mbali mbali wa maendeleo waliojitolea kusaidia vifaa mbali mbali vya ujenzi kwa Imani yao kwa wananchi hao pamoja na kuisaidia Serikali katika kuwafariji waathirika hao.
Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Serikali ya Wilaya, waheshimiwa wabunge na wawakilishi pamoja na Kamisheni ya kukabiliana na Maafa kwa hatua za haraka walizochukua ikiwa pamoja na kuwapatia chakula na kufanya tathmini ya awali kwa waathirika hao.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Muhamed Mahmoud ameeleza kuwa upepo huo umetokana na mabadiliko ya tabia Nchi na kueleza kuwa ni vyema Wananchi kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wakati wa ujenzi wa nyumba zao.
Aidha Mhe. Ayoub amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kufuatilia kwa karibu tokea kutokea kwa maafa hayo hatua ambayo imepelekea wananchi kuendelea kujenga Imani na Serikali yao.
Nao wananchi walioathirika na upepo huo wamemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kufika kuwafariji katika kipindi hichi kigumu na kueleza kuwa hatua hiyo inaonesha namna Serikali ya Awamu ya Nane inavyowajali wananchi wake.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekabidhi Mabati Thamanini (80) kwa ujenzi wa Mskiti ulioathirika uliopo Shehia ya Kigongoni pamoja na kupokea Mabati Hamsini (50) yaliyotolewa na Mzalendo ndugu Makame Simai (Chakua) kwa ajili ya kuwafariji waathirika hao.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
10/04/2023
No comments:
Post a Comment