Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Aendelea na Ziara Yake Pemba


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawekea mazingira mazuri wanamichezo kwa kujenga viwanja vyenye hadhi ya kitaifa na kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo wakati alipokagua matengenezo ya uwanja wa mpira wa miguu Gombani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

 

Amesema Serikali imedhamiria kukuza sekta ya michezo nchini ikiwemo kujenga viwanja mbali mbali vya michezo kila Wilaya  vyenye hadhi na viwango vya kitaifa na kimatifa ili kuondosha uhaba na changamoto za viwanja vya michezo hatua ambayo imepelekea kufanyiwa matengenezo makubwa kiwanja cha Gombani Pemba ili wananchi wanaokitumia waweze kuwa na mazingira mazuri ya Michezo kwa kuandaa na kuimarisha vipaji vyao.

 

Mhe Hemed amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kukaaa na mkandarasi anaesimamia shughuli za matengenzo ya uwanja huo kutatua changamoto zote zinazawakabili ikiwemo kusimamia mkataba wa matengenezi hayo ili aweze kumaliza kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.

 

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekutana na kufanya mazungumzo na wazee wa CCM Pemba pamoja na kuwagaiwa futari na kuwahakikishia kuwa Serikali ya mapinduzi ya zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuzingatia maslahi yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali inaendelea kukuza uchumi wake kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo kuimarisha miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege  ili kuimarisha huduma za kibiashara  na usafirishaji kwa wananchi na wageni.

Aidha amefafanua kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo na kueleza kuwa wananchi watakaoathirika kwa kupisha miradi hiyo watalipwa fidia zao kwa mujibu wa tathmini itakayofanyika.

Nao wazee wa Chama Cha Mapinduzi Pemba wamemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uamuzi wa kuwapatia Iftari katika kipindi hicho cha mwezi mtukufu wa ramadhani na kuwaombea Dua Viongozi wa Serikali ya Awamu ya nane ili waweze kufikia malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amegawa futari kwa wanafunzi wanaokaa Dhakalia za Skuli ya Fidel Castro Wilaya ya chake chake, Chuo cha Kiislamu Kiuyu mbuyuni Wilaya ya Micheweni na Skuli ya Utaani Wilaya ya Wete na kueleza kuwa ameamua kutoa Iftari hiyo ili wanafunzi na walimu wao  kuwa na utulivu katika masomo na hatimae kupata matokeo mazuri yatakayosaidia kufikia malengo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Nae waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohamed Mussa amemshukuru Mhe. Hemed kwa kutoa futari kwa wanafunzi wanaokaa Dakhalia wa Skuli hizo hatua ambayo inaonesha kuguswa kwake kuona Zanzibar inazidisha ufaulu kwa kiwango cha juu.

Amesema Jengo la Skuli ya Utaani lililoungua moto mwaka jana ambalo lilikuwa la ghorofa moja Serekali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeamua kujenga jengo la ghorofa tatu lenye Madarasa arobaini na moja (41), Maabara na Maktaba za kisasa , Chumba cha Kompyuta, Ofisi za Walimu pamoja na ukumbi wa Mikutano ambapo fedha za ujenzi huo zimeshatengwa na muda wowote atakabidhiwa mkandarasi kwa kuanza ujenzi huo.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amefika kujionea namna kituo cha kulelea yatima cha Daarul Ahbaab Micheweni na kuwapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa kuendelea kuwalea watoto hao kwa kusimamia malezi mema na kugawa futari pamoja na kuahidi kutatua changamoto zinazoikabili kituo hicho.


Katika ziara hiyoi Mhe. Hemed alifika katika ofisi za CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba kugawa futari kwa watendaji wa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake ambapo amewataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba na Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

08/04/2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.