RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kusisitiza
dhamira yake njema ya kuiunganisha tena Zanzibar kuwa moja yenye amani, upendo,
maridhiano na mshikamo.
Ameyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozindua tena Kamati ya Maridhiano baina ya Chama cha Mapinduzi na
ACT Wazalendo ifanyekazi pamoja kuendeleza amani iliyopo nchini.
Alisema bado ana nia
ya kuiendeleza Zanzibar kuwa moja bila kujali rangi, asili, imani za dini, au
itikadi za kisiasa kama alivyoahidi kwa mara ya kwanza alipohutubia Baraza la
Wawakilishi mwezi Novemba, 2022 juu ya dhamira yake ya kuwaunganisha wananchi
wa Zanzibar kuwa wamoja.
Alisema mara baada ya
uchaguzi wa mwaka 2020 waliendeleza tena Serikali ya Umoja wa kitaifa kwa
mujibu wa Katiba ya Zanzibar kama ilivyoelekeza, kwa nia ya kuweka jukwaa la
kutafuta suluhu ya kudumu ili kujenga maridhiano endelevu na amani ya kudumu
Zanzibar aliyoeleza kuwa ni njia pekee ya kujenga uchumi imara, kuondoa
umasikini na kujenga nchi kwa ustawi wa wananchi.
Rais Dk. Mwinyi, alitumia
fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kwake kwa vitendo
azma ya kuleta maridhiano ya kisiasa nchini ikiwemo kuunda kikosi kazi
kilichopitia ripoti ya mkutano wa Baraza la vyama vya siasa na kutoa
mapendekezo.
Pia Dk.
Mwinyi alimshukuru Dk. Samia kwa uzalendo wake wa kufanya vikao na viongozi wa
vyama vya siasa kwa kusikiliza maoni yao na kuyafanyia kazi.
Dk. Mwinyi ambae ni
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) Zanzibar alikishukuru Chama cha
ACT Wazalendo, kwa kukubali kukaa pamoja na viongozi wa CCM ili kuendeleza
dhamira ya kushirikiana na kuimarisha Umoja wa Kitaifa.
Awali, mwaka 2010
kuliwahi kuundwa Serikali ya Umoja wa kitaifa kufuatia mifarakano ya kisiasa na
jamii ikiwemo kuzorota kwa amani mara baada ya kuundwa kwa vyama vingi vya
siasa mwaka 1992 ambapo uchaguzi tangu mwaka 1995 na miaka iliyofuata Zanzibar
kuliibuka fujo za kisiasa na amani kudorora.
Kufuatia marekebisho
ya 10 ya katiba ya Zanzibar, Mwaka 2010 kuliundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
ili kuendeza amani ya kudumu.
Hafla ya uzinduzi wa
Kamati ya Maridhiano baina ya Chama cha Mapinduzi na ACT Wazalendo ilihudhuriwa
na viongozi wakuu na wajumbe kutoka vyama viwili hivyo, wakiwemo Makamu Mwenyekiti
wa Chama cha ACT Wazalendo kwa upande wa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu
ya Chama Cha Mapinduzi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed
Suleiman Abdulla, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar Dk. Muhamed
Said Dimwa, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM, Dk. Khalid Salum Muhamed ambae
pia ni Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi.
Wengine Vuai Ali Vuai
ni Mstaafu Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar pia ni Mjumbe kutoka CCM, Najma Murtaza
Giga mjumbe Halmashauri kuu Taifa na Mjumbe wa kamati ya maridhiano kutoka CCM,
Salum Hassan Bakari Mjumbe kutoka CCM.
Wengine ni Naibu
Katibu Mkuu ACT Wazalendo Zanzibar ambae pia ni Waziri wa Afya wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, Omar Said Shaaban Mwanasheria Mkuu
wa ACT ambae pia ni Waziri wa Biashara, Mansour Yussuf Himid, Mjumbe Kutoka ACT
Wazalendo na Ismail Jussa Ladhu Mjumbe wa Kamati Kuu ACT Wazalendo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment