Habari za Punde

TAMWA Zanzibar inaomba vyama vya siasa kuunga mkono juhudi za wanawake wenye nia ya kushiriki katika uongozi

 

CHAMA cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kinawataka Wanawake kuwa wajasiri na kujitayarisha kiuongozi bila kuogopa changamoto zinazowakabili wanawake wanapoingia katika uongozi ili kuongeza ushiriki wao kwenye vyombo vya maamuzi.


Idadi ndogo ya wanawake katika vyombo vya maamuzi na michakato ya kidemokrasia umekuwa ukijidhihirisha katika chaguzi zinazofanyika nchini kila baada ya miaka mitano ambapo wanawake hupata nafasi chache na ndogo jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa Tanzania kutokomeza umaskini na kuimarisha demokrasia inayowapa wananchi haki ya kuchagua kiongozi wamtakae. 


Hivi karibuni TAMWA ZNZ kimeendesha mafunzo kwa wanawake wenye dhamira ya kugombea nafasi za uongozi Zanzibar na kubaini kwepo kwa hofu miongoni mwa wanawake kushiriki katika nafasi hizo kutokana na sababu mbalimbali.


Miongoni mwa sababu zilizobainika kukwamisha ushiriki wa wanawake katika vyombo hivyo ni vitisho, hofu dhidi ya rushwa ya Ngono, pamoja kukosekana kwa mifumo na sera ya jinsia ndani ya vyama vya siasa inayowajenga na kuwaandaa wanawake kuwa viongozi bora.


Kukosekana kwa mifumo hiyo kunaathiri uwezo wa wanawake kutambua na kusimama kudai haki zao za msingi jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya katiba na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za kibinaadamu.


Aidha ilibainika kuwa changamoto hiyo inapelekea wanawake wengi kujaribu kuingia bila kuwa na misingi sahihi ya namna ya kuwa kiongozi bora na kuweka ugumu wa ufikiaji wa lengo namba tano la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohimiza upatikanaji wa Usawa wa Kijinsia kwa Wanawake na Wasichana katika nyanja zote.


Ikumbukwe kuwa kwa kutambua umuhimu wa mwanamke Sheria na sera mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi, Katiba ya Zanzibar ya 1984  kifungu 21(2) Kila Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke na  Taifa lake. 


Hivyo, TAMWA-ZNZ inaviomba vyama vya siasa na wadau wote kushirikiana kuwa mstari wa mbele kuwaandaa watoto wa kike katika misingi ya uongozi bora ili wakue katika misingi hiyo itakayowawezesha kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika michakato yote ya maamuzi kwa maendeleo ya Taifa.


Tunaamini kwamba uwepo wa sera  ya jinsia  ndani ya vyama   vya siasa  na kuweka  mifumo mizuri  ya miundo  ya uongozi inayozingatia jinsia itapelekea  kuwepo  kwa uwiano   wenye kutetea haki na maslahi ya makundi yote kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.


Ikumbukwe jumla ya wanawake 170   kutoka  Unguja   na Pemba wamejengewa uwezo kuhusu uongozi  kwa lengo la kufikia usawa wa kijinsia na kuengeza ushiriki wao katika   ngazi   za  maamuzi.


Tunaamini kwamba iwapo wanawake watajengewa misingi ya uongozi bora mapema itasaidia kupatikana kwa viongozi bora wenye kutetea haki na maslahi ya makumdi yote kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.


Pia tunawahimiza wanawake kuondoa hofu na badala yake wawe na uthubutu wa kushiriki kudai haki zao ikiwemo kujitokeza katika michakato ya uongozi ili kuwezesha upatikanaji wa usawa wa kijinsia.


Imetolewa na,

Idara ya Habari na mawasiliano

TAMWA Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.