23 Julai, 2023
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi amewata wakulima wa Mwani na wajasiriamali kuongeza juhudi
zaidi ya ukulima mwani na usarifu wa zao hilo, ili kuongeza tija na faida ya zao hilo.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo ukumbi wa Golden Tulip,
Uwanja wa ndege Zanzibar, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Mwani
duniani.
Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeanzisha kampuni ya
Mwani ya Serikali (ZASCO) ili kuleta matumaini ya kumkomboa mkulima wa mwani, kuongeza
bei bora kwa wakulima wa zao hilo.
Alisema, kilimo cha mwani ni utekelezaji wa mipango ya serikali katika kuleta mageuzi
kwenye sekta ya mwani nchini, kupitia uchumi wa buluu, juhudi zaidi
zimeongezeka na kueleza kuwa Serikali imevutiwa na jinsi ya wakulima wa zao
hilo na wananchi kwa ujumla wanavyoendelea kuitikia wito wa kauli mbiu ya
Serikali na kupata mwamko zaidi katika kuzichangamkia fursa za maendeleo na
ajira zinazotokana na kilimo na usarifu wa zao la mwani.
“Nakuhakikishieni Serikali yenu ipo pamoja nanyi
ili kuhakikisha zao la Mwani linaendelea kuwa mkombozi wa kuleta ustawi kwa
wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini kama tulivyodhamiria” aliahidi
Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi alieleza, mafanikio makubwa
yamepatikana kutokana na kilimo cha mwani kupitia fedha za Mfuko wa Ahuweni ya
UVIKO 19, Serikali imewasaidia wakulima wa mwani 5,000 kwa Unguja na Pemba kwa
kuwapatia boti maalumu zenye uwezo wa kufika kina kirefu cha maji na kuhimili athari
za mabadiliko ya tabianchi na ugonjwa wa ice-ice.
Alisema, licha ya mafanikio hayo ya utekelezaji wa
Sera na mikakati ya Wizara ya Uchumi wa bluu na mikakati ya uzalishaji wa mazao
ya baharini ukiwemo mwani, Serikali imewekeza fedha nyingi kuwasaidia wakulima
na wajasiriamali wa Sekta ya Mwani.
Pia, aliwashukuru wakulima wa mwana na wananchi
kwa kuifanya Zanzibar kuwa mzalishaji namba moja wa barani Afrika licha ya
changamoto za UVIKO – 19, mabadiliko ya tabia nchi, ugonjwa wa ice-ice, athari
za kuporomoka kwa bei ya mwani duniani, bado Zanzibar ina mchango mkubwa wa
uzalishaji mwani, kwa kushindana na wazalishaji wakubwa duniani kama China,
Philippines, Indonesia na wengine.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti
wa Kongano la Mwani, Zanzibar
(ZaSCI) Dk. Flower Msuya aliomba ushirikiano kutoka serikalini na taasisi zake
ili kuzimaliza changamoto zinazozikabili zao la mwani nchini.
Alieleza, changamoto
tabianchi na bei ndogo ya zao hilo zimelisababisha kuanzishwa kwa Kongano la
Mwani miaka nane iliyopita, ili kuleta ubunifu na usarifu wa mwani Zanzibar.
Dk. Flower alieleza Zanzibar
kwa mara ya kwanza ilitambua bidhaa zinazotokana na zao la mwani mwaka 2006 kwa
kikundi cha kwanza wanawake na kinamama kutoka Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja
kuwapa elimu ya kusarifu bidhaa za zao la mwani kwa matumizi mengine ya jamii.
Kwa muijibu wa takwimu za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, uzalishaji mwani umeongezeka kutoka tani 9,663 mwaka 2019/2020, na
kufikia tani 12,594 mwaka 2021/2022.
Zao la mwani lina matumizi mengi kwa usatawi wa
uchimi wa Zanzibar ikiwemo chakula, vipodozi, dawa, mbolea na chakula cha
mifugo.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment