Habari za Punde

Wakaguzi wa Ndani Wapatiwa Mafunzo Ili Kuboresha Taarifa za Fedha


Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Benjamini Magai, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya ukaguzi wa taarifa za fedha kwa Wakaguzi wa Ndani, yaliyofanyika Ofisi ya Hazina, Dar es Salaam.

Na. Josephine Majura, WF, Dar es Salaam.

Jumla ya wakaguzi 120 wa ndani wa taarifa za fedha wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukagua taarifa za fedha ili kuhakikisha taarifa za fedha zinaandaliwa kwa viwango vya kimataifa.

Akizungumza wakati wa Kufunga mafunzo hayo, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Bw. Benjamin Magai, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuboresha utendaji wa wakaguzi wa ndani ili kuzishauri menejimenti za taasisi husika kuhusu usahihi wa taarifa hizo kabla hazijawasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Bw. Magai, aliongeza kuwa Taarifa za fedha zinapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu na miongozo ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi ikiwa ni pamoja na kupunguza hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na CAG.

"Ni matarajio yangu kuwa kupitia mafunzo haya mtakuwa mmeelewa namna bora ya kukagua Taarifa za Fedha za taasisi zenu hali itakayopelekea kutoa ushauri stahiki utakaowezesha kuboreshwa kwa taarifa husika kabla ya kukamilika kwa ukaguzi wa CAG”, alisema Bw. Magai.

Aidha, Bw. Magai aliwataka wakaguzi waliohudhuria mafunzo hayo kupeleka pia ujuzi kwa wale ambao hawakuweza kushiriki waweze kupata maarifa na kufanya vizuri katika taasisi zao na Wizara kupitia ofisi ya Mkaguzi wa ndani mkuu wa serikali itafanya ufuatiliaji wa ufanisi wa ukaguzi wa taarifa hizo kwa taasisi zote ambazo zimepatiwa mafunzo ili kutathmini utekelezaji wa jukumu hilo.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa awamu mbili ambapo kila awamu ikiwa na wakaguzi wa ndani 60.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu Msaidizi Bw. Emanuel Subi akimkaribisha Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Benjamini Magai, kufunga mafunzo ya ukaguzi wa taarifa za fedha kwa Wakaguzi wa Ndani yaliyofanyika Ofisi ya Hazina, Dar es Salaam.
Wakaguzi wa Ndani, wakifuatilia hotuba ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Benjamini Magai (hayupo pichani), wakati akifunga mafunzo ya ukaguzi wa taarifa za fedha, yaliyofanyika Ofisi ya Hazina, Dar es Salaam.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Benjamini Magai (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa taarifa baada ya kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika Ofisi ya Hazina, Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WFM – DSM)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.