Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewapongeza Wabunge wa Zanzibar kwa
kutumia vyema nafasi zao za uwakilishi wa majimbo yao ambapo juhudi hizo zimewezesha
utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Agosti 24, 2023, wakati
wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria
kilichopokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu
wa Rais katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema juhudi kubwa
zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Nane inayoongozwa
na Mhe. Rais Dkt. Hussein Ally Mwinyi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
kwa wananchi imetokana na mshikamano mkubwa unaofanywa na Wabunge wa Zanzibar
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusemea na kutetea hoja
mbalimbali.
“Leo hii ndani ya miaka miwili ya Uongozi wa Serikali
ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Nane, Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi tumeshuhudia
mageuzi makubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi...Juhudi
hizi zimetokana na ninyi Wabunge katika kujenga hoja Bungeni” amesema Dkt.
Jafo.
Waziri Jafo amesema katika kipindi cha miaka miwili ya
Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea
kupokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
huku akitolea mfano fedha za miradi ya UVIKO 19 ambazo zimetekeleza miradi ya
sekta muhimu za kijamii kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, maji na barabara.
Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema malengo ya Viongozi
Wakuu wa Serikali ni kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayogusa maisha ya
wananchi inatekelezwa kwa kasi na viwango ili kuwaletea maendeleo ya wananchi
na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao Wajumbe wa kamati hiyo, wameipongeza
Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha na kutoa mafunzo ya Sheria ya Mfuko wa Kuchochea
Maendeleo ya Jimbo ambao umeainisha wajibu na nafasi ya Wabunge na Watendaji wa
Halmashauri katika kusimamia Mfuko huo.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Ahmed
Juma Ngwali aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha mafunzo ya Sheria
ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo mwezi Julai mwaka huu na sasa mafanikio ya
mafunzo hayo yameanza kuzaa matunda na kuleta mabadiliko kwa wasimamizi na
watendaji wa mfuko huo.
“Tunakushukuru Mhe. Waziri Jafo kwa
kufanya ziara Zanzibar mwezi Julai mwaka huu na zaidi ni yale mafunzo
yaliyotolewa na Ofisi yako kuhusu Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya
Jimbo kwa sisi Wabunge na Watendaji wa Halmashauri kwa upande wa Zanzibar na
PEMBA…Mambo sasa yamebadilika na tunakwenda vizuri” amesema Ngwali.
Aidha Ngwali amesema kabla ya
mafunzo hayo, kulikuwa na mkanganyiko kuhusu usimamizi wa fedha hizo jambo
lililokuwa likizua malalamiko na lawama kwa watendaji na wasimamizi
kuchelewesha fedha katika majimbo na pia na Viongozi kutofahamu taratibu
zinazotumika katika ugawaji, utoaji na na upatikanaji wa fedha hizo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha Ngwali aliipongeza Serikali ya
Awamu ya Sita kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maendeleo
Zanzibar na kutolea mfano fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa
Uwanja wa Ndege Pemba na ukarabati wa ujenzi wa barabara ya Wete-ChakeChake
ambapo kiasi cha TZS Trilioni 1.4 zimetengwa kutekeleza miradi hiyo.
Nae Mjumbe mwingine wa Kamati hiyo, Mhe.
Abdullah Ally Mwinyi ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa juhudi kubwa
inazoendelea kuzifanya katika kuendelea kutoa mafunzo usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo
ya Jimbo na kueleza kuwa mafunzo hayo yatawezesha kuongeza ufanisi katika
usimamizi na uendeshaji wa mfuko huo ambao umekusudia kutekeleza miradi inayoibuliwa
na wananchi katika Majimbo.
Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyotungwa na Bunge, ambapo Fedha za Mfuko hutolewa katika Majimbo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyopitishwa kisheria.
No comments:
Post a Comment