Habari za Punde

Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, washirikiane na wadau wengine kuendelea kulitangaza zao la mwani kitaifa hadi kimataifa

MWENYEKITI wa Bodi ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mke wa Rais wa Zanzibar. Mama Mariam Mwinyi ameiomba Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, washirikiane na wadau wengine kuendelea kulitangaza zao la mwani kitaifa hadi kimataifa ili kuliongezea soko kwa ajili ya wakulima wa ndani na kujulikana duniani kote.

Mama Mariam Mwinyi, alieleza hayo alipokabidhi vifaa vya kuanikia mwani kwa wakulima wa mwani Zanzibar kwenye uwanja wa mpira wa Bweleo, Wilaya ya Magharibi 'B', Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema, mwani huimarisha ustawi wa jamii kwa kupugunza vifo vya mama na watoto vinavyotokea wakati wa uzazi kutokana na wajawazito kupata matatizo ya upungufu wa damu.

Katika hatua nyengine Mama Mariam Mwinyi amewashauri wanawake kuongeza matumizi ya bidhaa zinazotokana na zao la mwani kutokana na virutubisho vingi vilivyomo kwenye zao hilo vinavyoimariisha afya hasa ya mama wajawazito ambavyo ni nadra kupatikana kwenye mazao mengine.

Pia, Mama Mariam aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuipa kipaumbele sekta ya uchumi wa buluu wanaoshughukila sekta ya mwani nchini ambayo inasaidia kuwakomboa wakulima wengi wa zao hilo.

Mbali na faida nyingi za mwani alizozitaja pia alieleza zao la mwani hutoa virutubisho vingi vinavyosaidia binaadamu kuliko virutubisho vinavyopatikana kwenye mazao mengine, hivyo aliwaomba vijana kuitumia fursa ya kilimo cha mwani iliyopo kujinufaisha kiuchumi.

Sambamba na hayo Mama Mariam aliisihi jamii ya Wazanzibari waendelee kutumia bidhaa asili hasa zilizotokana na zao la mwani.

Pia aliwanasihi wasarifu wa zao hilo, kujitahidi kuziboresha bidhaa za mwani kwenye usafi wa hali ya juu kwani hutumiwa kama chakula, mbolea, dawa, vipodozi vya ngozi na kuimarisha nywele.

Aliisifu Zanzibar kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa ubora wa kilimo cha mwani na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ya kilimo hicho na kuendelea kushika kasi ya uzalishaji wa zao hilo duniani kote. 

Hata hivyo, Mama Mariam Mwinyi aliwasihi wakulima hao kuvitunza vyema vifaa hivyo ili vidumu muda mrefu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Baluu na Uvuvi, Dk. Suleiman Aboud Jumbe, aliipongeza Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kwa juhudi ya kuwasaidia kinamama na vijana kwenye  nyanja mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kuongezea nguvu ya kuwagawia vifaa vya ukulima mwani katika kuendeleza kilimo hicho nchini ambacho kitaleta mabadiliko chanya ya kuinua sekta ya mwani kwenye sekta ya uchumi wa bluu.

Naye, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Nyabenyi Tipo, aliahidi kuendelea kuwasaidia wakulima wa zao la mwani nchini na kuongeza ushirikino na kuendelea kuungamkono harakati za  maendeleo kwa serikali zote mbili za SMZ na SMT.

Sambamba na kusifu mchango mkubwa unaotolewa na ZMBF katika kuisaidia jamii ya Wazanzibari husuasani kina mama wa mwani.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Fatma Fungo, alisema tayari taasisi hiyo imewaunga mkono kinamama na vijana kutoka vikundi 18 vya wakulima wa mwani kwa Unguja na Pemba, ikiwemo kuwapatia vifaa vya kisasa vya ukulima wa zao hilo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30, zikiwemo boti za ‘fiber’ tisa zenye urefu wa mita tano na mashine zenye uwezo wa 9.9 HP , nanga, mashine za kusagia mwani, mashine za kukorogea sabuni na vifaa vyengine vya kusarifu mwani pamoja na maboya ya ukozi.

Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) iliasisiwa Julai mwaka 2022 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka jana na mwezi Machi mwaka huu, ilizindua Mpango Mkakati wa miaka mitatu pamoja na mradi wa “Tumaini kit” ambao hadi sasa tayari umefanikiwa kuzalisha taulo za kike zaidi ya 5000 na kuzisambaza zaidi ya 1500 kwa wanafunzi na wasichana wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.

Aidha, taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.