Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.3 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.1 kwa mwaka 2022 kutokana na maboresho yaliyofanywa katika usinamizi wa Sekta hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa kufunga maonesho ya sita ya Teknolojia na uwezeshaji katika Sekta ya madini yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo cha uwekezaji cha Bombambili Mkoani Geita.
Amesema kuboreshwa kwa usimamizi wa Sekta ya madini na kuweka mazingira wezeshi ya biashara ambayo inaongeza mchango wa kupatikana ajira kwa wananchi pamoja na kandarasi zinazotolewa na Migodi imepelekea kuwa ni miongoni mwa Sekta inayosaidia kukuza Uchumi wa Tanzania.
Amesema Maonesho hayo ni miongoni mwa mkakati unaotoa matarajio makubwa ya kuona Sekta ya Madini inaongeza mchango wake katika uchumi wa Nchi kwa maendeleo endelevu ya watanzania.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa lengo la Sera ya Madini nchini ya mwaka 2009 ni kuhakikisha kuwa Sekta hiyo inafungamana na Sekta nyengine za kiuchumi ikiwemo Sekta za Fedha, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mawasiliano, usafirishaji, wazalishaji na wasambazaji wa Malighafi ili kuleta tija na maendeleo ya haraka hasa ajira zinazotokana na shughuli zinazotokana na Sekta ya Madini hatua ambayo itasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi Nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka Wachimbaji wa madini kuendana na Teknolojia kwa kutumia vifaa na Teknolojia ya kisasa ili kusaidia kukuza kipato cha wachimbaji wadogo na kupelekea kukuza Pato la Taifa na kuhifadhi mazingira katika Shughuli zao.
Sambamba na hayo Rais. Dkt. Samia amezipongeza Taasisi mbali mbali za kifedha kwa kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini na wajasiriamali kuhusu upatikanaji wa fursa mbali mbali za utoaji huduma katika Migodi, mitaji na usimamizi wa fedha za biashara jambo ambalo litasaidia kutatua changamoto ya kukosa mitaji na nanma bora ya kuweka kumbukumbu za gharama na uzalishaji.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Migodi mitatu ya usafishaji wa Madini ya fedha na dhahabu imejengwa Mikoa ya Dodoma, Mwanza na Geita yenye uwezo wa kusafisha Kilo 965 kwa siku itakayowezesha madini ya dhahabu na fedha kusafishwa kwa asilimia 99.99 na kupata thamani halisi ya madini hayo.
Aidha amewataka wachimbaji wa madini kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha shughuli za madini zinakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira ili kuwa na uchumbaji salama kwa wananchi.
Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wachimbaji wa madini wanapata masoko ya uhakika na itaendelea kuwawezesha wawekezaji wadogo wa Sekta ya madini kwa kuwaunganisha na Taasisi za kifedha.
Pamoja na hayo ameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kununua dhahabu ili Tanzania iweze kuwa na akiba ya dhahabu ya kutosha na kuimarisha shilingi ya Tanzania na Uchumi. |
Nae Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa Wizara itaendelea na Mkakati wa kuyaendeleza Madini Mkakati na madini muhimu kuendana na Dunia ili kuwa na Madini safi pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya wananchi waweze kunufaika kupitia sekra ya Madini.
Ameeleza kuwa Maonesho hayo yanaenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza Sekta ya madini yenye mchango mkubwa wa kukuza Uchumi wa Tanzania.
Akisoma taarifa fupi juu ya maonesho ya madini kwa mwaka 2023 Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Mohd Gumbat amesema maonesho haya yametoa fursa mbali mbali kwa wachimbaji, wachenjuaji na wadau wa madini nchini kama vile mafunzo juu ya namna bora za kupata mitaji katika sekta za fedha, matumizi ya Teknolojia ya kisasa pamoja na kutambua fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya madini.
Aidha amesema kwa vile maonesho haya yanatoa fursa ya kujitangaza kwa wachimbaji wakubwa, wakati na wadogo Serikali kupitia Wizara ya Maadini wameona ipo haja maonesho haya kuwa endelevu na kufanyika kila mwaka.
Akitoa salamu za Chama cha Wachimbaji wadogo wa Madini (FEMATA) Bi Semeni John Malale Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wachimbaji Tanzania ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea mazingira mazuri wachimbaji wadogo hasa kuwatafutia Soko ndani na nje ya Nchi.
Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembelea Mabanda mbali mbali ya maonesho yaliyoandaliwa na Wadau wa madini ambao kwa pamoja wamemuahidi Mhe. Hemed kuwa wataendelea kudhamini maonesho hayo kwa kuwawewezesha wachimbaji wadogo na wachenjuaji wa madini ili kuiwezesha Sekta hiyo kuzidi kuimarika.
Wamefahamisha kuwa Sekta ya madini inahitaji Teknolojia ya kisasa, fedha, elimu na mikopo kwa Wachimbaji wadogo wa madini hivyo, wataendelea kushirikiana na Serikali kuona kuwa Sekta ya madini ni Sekta moja wapo inayochangia Pato la Serikali na kuinua Uchumi wa Nchi.
No comments:
Post a Comment