Habari za Punde

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi ashiriki Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Jumuiya za Uvuvi Duniani(ICFC) nchini Korea ya Kusini



 Mheshimiwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mheshimiwa Suleiman Masoud Makame ambaye yupo Korea, akiongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Jumuiya za Uvuvi Duniani(ICFC) unaofanyika Mji wa Bandari wa Busan, ameipongeza Jumuiya hiyo kwa juhudi na jitihada zao kubwa za kuwaunganisha wavuvi wadogo wadogo ulimwenguni na katika kuleta ufumbuzi endelevu wa changamoto mbali mbali za kiuchumi, kijamii, zana na miundombinu imara kwa ajili yao.

Pia amegusia haja ya uwepo wa mashirikiano zaidi ya pamoja katika kukabiliana na majanga ya mabadiliko ya tabia nchi, uchafuzi wa mazingira ya bahari, kupungua kwa mavuno ya samaki, na uwezo mdogo wa kijasiriamali, yanayowakabili wavuvi wadogo wadogo ulimwenguni.
Aligusia pia suala la umuhimu wa uwezeshaji wa jumuiya za wavuvi wadogo wadogo ulimwenguni katika uvuvi wa kisasa, na maendeleo ya mazao ya baharini kwa jumuiya za wavuvi ulimwenguni ikiwemo Tanzania.
Mkutano huu utafikia kilele hapo kesho tarehe 21 Septemba 2023. Wakati huo huo Mheshimiwa Waziri Suleiman Masoud Makame amesifu mahusiano makubwa na ya karibu kabisa yaliyopo baina ya Korea na Tanzania na hasa katika Uvuvi na Sekta nyengine za Uchumi wa Buluu. Alisema hayo alipokuwa akifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Taasisi ya Masuala ya Bahari ya Korea (KMI) Kim Jong-Deoug.
Mheshimiwa Waziri amepongeza pia jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Ubalozi wa Tanzania wa Seoul, za kuvutia wawekezaji kutoka Korea na hususan katika sekta za Uvuvi, Mwani, Bandari, Utalii, Nishati n.k na kwamba Tanzania, ikiwemo Zanzibar, imekuwa ikifaidika sana na matunda ya mashirikiano hayo.
Akiwa Korea Mheshimiwa Waziri amepokelewa na Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mheshimiwa Togolani Mavura.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.